MFUKO wa Bima ya Afya ya Jamii ulioboreshwa ( iCHF), umefanikiwa kukusanya kiasi cha zaidi ya Shilingi bilioni 30 kutokana na michango ya wanachama wake kwa kipindi cha miaka minne hadi 2022.
Kati fedha iliyokusanywa Shilingi bilioni 20 zimerejeshwa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya yakiwa ni malipo ya gharama za kuhudumia wanachama.
Mratibu wa mfuko wa iCHF kutoka Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ( TAMISEMI), Silvery Maganza alisema hayo Desemba 5, 2022 mjini Morogoro wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo maofisa wa mfuko ngazi ya mikoa ambao ni wahasibu , wataalamu wa Tehema na waratibu yaliyohusu matumizi ya mfumo wa ulipaji serikalini (MUSE).
Mafunzo hayo yamefadhiliwa na serikali ya Uswis chini ya Shirika la Maendeleo ya Ushirikiano la Uswis (SDC) kupitia Mradi wa HPSS Tuimarishe Afya (Health Promotion and System Strengthening).
Amesema mfuko huo una zaidi ya wanachama milioni nne sawa na asilimia 7.6 na kwamba lengo ni kufikia asilimia 80 ya Watanzania walio kwenye sekta zisizokuwa rasmi ambao mara nyingi wanapata changamoto ya matibabu kwa kukosa fedha wanapougua.
Maganza amesema icha ya idadi ya wanachama walioandikishwa ni ndogo, hilo linatokana na elimu ndogo kwa wananchi ya kutambua faida ya mfuko huo na umuhimu wake katika jamii.
“ Nitumie fursa hii kuwaomba wananchi kujiunga na mfuko huu ili wawe na uhakika wa matibabu , wanapaswa kujua ugonjwa unakuja bila ya taarifa , ni umuhimu kwao kuchangia malipo ya iCHF ili ikitokea mtu ameugua aweze kupata huduma ya matibabu” anasema Maganza.
Pia anasema mfumo wa tehema unaotumiwa kwa sasa umeonyesha mafanikio makubwa kwa kurahisisha kazi kwa vile mwananchi anaweza kujiandikisha kupata kadi na huduma za matibabu kuanzia ngazi ya nchini hadi hospitali za rufaa za mikoa popote pale nchini.
Naye mchambuzi wa mifumo ya Tehema kutoka Mradi wa HPSS Tuimarishe Afya ,Nicholas Kanisa amesema wakiwa ni wadau, kwa kushirikiana na serikali wanasaidia maeneo mbalimbali ya huduma za afya.
Amejata maeneo hayo ni pamoja na masuala ya kiufundi na kifedha ili kuhakikisha kwamba mifumo yote inaunganika ikiwa na uwezeshaji wa mafunzo kwa watumishi wa mfuko wa iCHF ya kuwajengea uwezo .