WANANCHI wengi hawana uelewa kuhusu masuala ya bima kwa kufikiria kuwa ipo kwa ajili ya matajiri pekee tofauti na uhalisia kuwa kila mmoja anapaswa kuwa nayo.
Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa Taasisi wa kampuni za Bima, Khamis Suleiman wakati wa uzinduzi wa ushirikiano wa mpango mahususi wa mafunzo maalum kwa tasnia ya bima Tanzania na Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) pamoja na Shirika la Kazi Duniani (ILO).
Amesema ili kutoa elimu hiyo mpango huo utaaanza kuwafundisha walimu ambao wataipeleka kwa wanaouza bima ambao nao wataipeleka kwa walengwa ambao ni jamii ya wakulima, wafugaji, mama lishe na watu wengine wenye shughuli ndogondogo.
“Malengo ya bima ni kuhakikisha walau ifikapo mwaka 2030 angalau asilimia 50 ya watu wazima Watanzania kila moja angalau awe na hata bima moja. Wengi wanadhani kuwa bima ni kwa ajili ya matajiri au wenye vipato vikubwa, lakini huu mkakati uliowekwa ni kuonesha kuwa hata watu wa kipato cha chini kabisa nao wanastahili na wanaweza kununua bima,” amesema.
Akizungumzia hilo Mwenyekiti Mtendaji wa Chuo cha Mambo ya Bima na Hifadhi za Jamii Afrika (ACISP), Sosthenas Kewe amesema chuo hicho kimezindua ushirikiano wa mpango mahsusi wa mafunzo maalum kwa tasnia ya bima hapa nchini kwa kushirikiana na UNDP pamoja na ILO.
Amesema mafunzo hayo ya kujenga uwezo kuhusu bima yanalenga kuongeza weledi, maarifa na ujuzi kwa watenda kazi wa kampuni za bima, simu, benki za Tanzania, taasisi zinazotoa mikopo, lakini pia na wasimamizi wa masoko ya fedha hasa katika eneo la bima.
” Mpango huu ni mahsusi kwa Tanzania kati ya chuo hiki na UNDP pamoja na ILO, likiwa na lengo la kuhakikisha kuwa tasnia ya bima inakuwa zaidi na kwa kasi.
“Tunajifunza kwamba tasnia ya bima bado haijawa na ukubwa unataotakiwa ili uweze kuleta mabadiliko ya kweli katika maisha ya Watanzania katika makundi mbalimbali kwa maana ya wakulima, wajasiriamali au wafanyabiashara, katika sekta ya afya, elimu na maeneo kama hayo,” amesema.