BINTI aliyekatisha masomo ya sekondari mjini Iringa baada ya kupata ujauzito na kisha kujifungua, amekatisha maisha yake kwa kujipiga kitanzi kwa kile kilichodaiwa kukosa matunzo yake yeye na mwanae na mizozo ya kifamilia.
Binti huyo Winfrida Mdindile (17) mkazi wa mtaa wa Semtema, mjini Iringa alikuwa mwanafunzi wa shule ya sekondari Kihesa ya mjini humo wakati akipata ujauzito huo, mwaka juzi.
Amejinyonga alfajiri ya kuamkia leo mpaka kufa na kuacha mtoto anayekadiriwa kuwa na mwaka mmoja.
Akizungumza katika eneo la tukio nyumbani kwa marehemu, Mama mzazi wa marehemu huyo, Agness Donald alisema mwaka jana binti yake huyo alipata ujauzito aliodai alipewa na mwanafunzi mwenzake na hivyo kulazimika kukatisha masomo yake akiwa kidato cha kwanza.
Alisema siku moja kabla ya tukio hilo lililothibitishwa na jeshi la Polisi, binti huyo aliaga anakwenda kutembea lakini tofauti na kawaida yake alichelewa sana kurudi nyumbani.
Akizungumza na wananchi baada ya tukio hilo Mkuu wa Kituo Kidogo cha Polisi cha Semtema, Cosmas Ngai alisema jeshi la polisi linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo.