Biteko atoa maagizo Wizara ya Maji

DODOMA: NAIBU Waziri Mkuu Dk Doto Biteko ametoa maagizo 10 kwa Wizara ya Maji ili kuboresha huduma na vyanzo vya maji nchini.

Akitoa maagizo hayo leo Machi 22,2024 katika ukumbi wa mikutano Mtumba mjini Dodoma, katika wiki ya kilele cha maji duniani yenye kauli mbiu ‘Uhakika wa Maji kwa Amani na Utulivu’ Biteko ameitaka Wizara ya Maji kuhakikisha wanatoa maoni hasa kwenye vyanzo vya kuhifadhi maj, uvunaji wa maji ya mvua na kuongeza ufanisi katika matumizi ya maji upewe kipaumbele kwenye dira ya taifa tunayoiendea.

Amesema, lengo ni tatizo hilo lionekane kwa ukubwa. Pili Wizara ya maji ihakikishe watanzania wengi wanapata huduma ya maji safi na salama.

“Tumejenga miundombinu kwa gharama kubwa ili miundombinu hiyo iweze kufikisha huduma ya maji, hatuna budi kuhakikisha kuwa tunavilinda vyanzo vya maji kwa wivu mkubwa,”amesema Biteko.

Pia, ameagiza maeneo yote yasiyo na vyanzo vya uhakika Wizara ijielekeze katika ujenzi wa mabwawa ya kuvuna maji ya mvua na miradi mikubwa ya kimkakati.

“Haya yote hayawezi kuanza kama hatujaamua, ni lazima tuanze sehemu fulani, unaweza kupata habari kwamba tunahitaji rasilimali ndio tujenge, mimi siamini hivyo, mimi naamini tuna hitaji moyo wa kujenga rasilimali zitatufuata njiani,”amesema Biteko

Agizo lingine alilotoa Biteko ni wizara kuhakikisha Taasisi za Bodi za Bonde kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kuongeza jitihada za kudhibiti uchafuzi wa mazingira.

“Tunapenda kuona uwekezaji lakini uwekezaji uwe na tija ya kulinda mazingira yetu na mazingira yetu yasiweze kuathirika na baadae tukapata madhara ya maji.”amesema

Aidha, Biteko ametoa wito kwa sekta binafsi kukuza ushiriki wao katika kutunza mazingira na usimamizi wa maji mijini na vijijini, kwa kile alichoeleza kuwa kuna mifano mingi ya wadau walioshiriki eneo hilo, lakini bado wanaomba wadau waendelee kuisapoti serikali kwa kuwa kuna kazi kubwa ya kufanya katika eneo hilo.

“Nitoe wito kwa kila kaya, taasisi za serikali, taasisi binafsi, madhehebu ya dini, hasasi zisizo za kiraia na kila mwananchi mmoja mmoja kuweka miundombinu ya kuvuna maji katika nyumba zao ili kuimarisha upatikanaji wa maji kutokana na mvua zinazonyesha.”amesema na kuongeza

“Pamoja na kuipongeza wizara kwa mtazamo chanya kwenye sekta ya maji na katika kutunza vyanzo vya maji, kutoa vibali vya kumwaga maji taka, kujenga miundombinu na ukarabati wa kuhifadhi takwimu za maji nawaagiza viongozi, wataalamu wote mliopo hapa kushirikiana na wizara kusimamia kikamilifu maeneo yote yenye vyanzo vya maji ili yale yote yaliyotengewa miundombinu yalindwe kwa kushirikiana na taasisi nyingine,”amesisitiza.

Habari Zifananazo

Back to top button