Biteko nyota inayong’ara

NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko anaingia katika historia ya viongozi wachache kushika wadhifa huo ambapo Dk. Salim Ahmed Salim alishika wadhifa wa Naibu Waziri Mkuu kuanzia mwaka 1984 – 1989 huku pia akiwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.

Mwingine ni Hayati Augustine Lyatonga Mrema alishika wadhifa huo kuanzia mwaka 1991- 1994 lakini pia alikuwa katika nafasi hiyo huku pia akiwa ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.
Dk. Biteko alizaliwa Disemba 30, 1978 ni mbunge wa Bukombe tangu mwaka 2015 hadi sasa kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Alianza elimu ya msingi mwaka 1988 na kuhitimu mwaka 1994 katika shule ya Nyaruyeye iliyopo mkoani Geita, baadae alijiunga na shule ya sekondari Sengerema kwa masomo ya kidato cha kwanza hadi cha nne kuanzia mwaka 1995 hadi 1998.

Mwaka 1999 hadi 2001 alijiunga na chuo cha ualimu Katoke na kusomea ualimu ngazi ya cheti, 2002 hadi 2004 alisomea sanaa za majukwaani katika ngazi ya cheti, chuo cha ualimu Butimba.

Baadaye mwaka 2004 hadi 2005 aliendelea na elimu ya kidato cha tano na sita katika shule ya ufundi Butimba huku mwaka 2005 hadi 2007 alijiunga na chuo cha ufundi Morogoro kwa ajili ya masomo ya ngazi ya stashahada, mwaka 2007 mwishoni alijiunga na Chuo Kikuu Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT) kusoma shahada ya ualimu aliyohitimu mwaka 2010.

Aliendelea na masomo ya shahada ya uzamili hapo hapo SAUT kuanzia 2011 na kuhitimu 2013 ambapo mwaka huo huo alijiunga na Chuo Kikuu cha Renmin cha nchini China kwa masomo ya Uongozi wa elimu katika ngazi ya cheti .

Akiwa katika mtumishi wa umma Biteko amehudumu katika nafasi mbalimbali za ajira katika utumishi wa Umma kuanzia mwaka 2002 hadi sasa ambapo amehudumu katika kipindi tofauti kwa nafasi ya ualimu Wilaya ya Geita, Ofisa Elimu wa Wilaya ya Nyanghwale 2013 hadi 2015, Naibu Waziri wa Madini mwaka 2017 hadi 2019, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Bunge mwaka 2015 hadi 2018.

Katika safari yake ya siasa alianza mwaka 2005 kwa nafasi ya Mjumbe wa Baraza la Vijana la Wilaya, mkoani Geita kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) baadaye harakati zikaendelea angali mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT) jijini Mwanza akihudumu nafasi ya ujumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi mwaka 2007.

Biteko ameendelea kuwa na ustawi mzuri katika duru za siasa na uongozi kwani mwaka 2010 alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Chama Cha Walimu wilaya ya Geita na baadae mwaka 2012 kupanda hadi Mwenyekiti wa Chama Cha Walimu Mkoa wa Geita nafasi aliyohudumu hadi 2015.

Hata hivyo, baada ya kujipima kuona anatosha ikambidi aombe ridhaa ya wananchi wa jimbo la Bukombe ili kuwatumikia katika nafasi ya ubunge, na wana Bukombe wakampa ridhaa kwa kumpa kura za kutosha katika Uchaguzi Mkuu wa 2015.

Akiwa bungeni nyota ya Biteko ilizidi kung’aa kwani alipata kofia mbili bungeni ambazo ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Bunge na Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini kuanzia mwaka 2015 hadi 2018.
Akiwa ndani ya kamati hizo mwaka 2017 akateuliwa na Hayati Rais Dk. Magufuli kuwa Naibu Waziri wa Madini na kufikia 2019 akateuliwa kuwa Waziri wa Madini nafasi aliyoendelea kuitumikia hadi 2020 Uchaguzi Mkuu ulipoitishwa.

Matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 yalimrudisha tena Biteko bungeni ambapo aliteuliwa tena kuwa Waziri wa Madini nafasi aliyohudumu hadi leo Agosti 30, 2023 Rais Dk. Samia Suluhu Hassan alipomteua kuwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati nafasi atakayohudumu rasmi atakapoapishwa Septemba Mosi, 2023 katika Ikulu ndogo ya Zanzibar.

Habari Zifananazo

7 Comments
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button