BMT wakabidhi bendera timu ya ngumi

DAR ES SALAAM: Baraza la Michezo la Taifa (BMT) limeiaga kwa kuikabidhi bendera ya taifa timu ya ngumi za wazi ya Tanzania katika safari ya kuelekea Senegal kushiriki mashindano ya kufuzu Olimpiki 2024, huko Paris Ufaransa.

Akikabidhi bendera hiyo kwa niaba ya Katibu Mtendaji Thadeus Almas, Mwanasheria wa BMT amewataka kwenda kuipigania nchi kufuzu kushiriki mashindano hayo na siyo kwenda kutembea.

Kwa upande wake mkuu wa msafara huo, Rais wa Shirikisho la Ngumi za Wazi la Tanzania OBFT, Lukelo Willilo amesema mashindano hayo yanatarajiwa kuanza rasmi Septemba 09-15 katika jiji la Dakar, Senegal.

Advertisement

“Tanzania itawakilishwa na wachezaji sita badala ya saba hii ni kutokana na mmoja kushindwa kukidhi viwango vya uzito. Kati yao wanawake ni wawili na wanaume wanne,”
“Kikosi hicho kitaongozwa na nahondha bondia Yusuph Changalawe, Joyce Mwakamele, Zulfa Macho, Mwalamu Salum Mohamed, Abdallah Salum Abdallah, pamoja na Mussa Mwalegesi” amesema Wililo.

Aidha, kikosi hicho kitaongozwa na Mwalimu Mkuu, Samweli Samwel Kapungu akiwa na wasaidizi wawili akiwemo Katibu Mkuu OBFT, Makore Mashanga.

Naye, nahodha wa kikosi hicho, Yusuph Changalawe amesema wamepata maandalizi mazuri hivyo hakuna maneno mengi isipokuwa kuhakikisha wanafuzu katika mashindano hayo.

“Napenda kujivunia serikali yangu kwa kutuwezesha katika safari yetu na sina mengi ila nawaahidi tulipoishia ndipo tutakapoanzia” amesema Changalawe.

7 comments

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *