BMZ yatakiwa kuboresha kitengo cha TEHAMA

ZANZIBAR: WATENDAJI  wa Baraza la Mitihani la Taifa (BMZ)  wametakiwa kuimarisha  nguvukazi katika maeneo muhimu ikiwemo kitengo cha Tehama ili  kuongeza ufanisi katika utendaji wao.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Lela Mohamed Mussa, katika  ziara yake katika Makao Makuu ya Baraza hilo zilizopo Vuga.

Amesema kuhimarishwa kwa mifumo ya Tehama kutaondoa  changamoto zilizopo na na kuwataka kufanya  kazi kwa bidii na ufanisi.

Advertisement

Aidha, amesisitiza juu ya umuhimu wa kutumia watu wenye ujuzi na uzoefu katika shughuli za upimaji na tathmini,  akihimiza ushirikiano kati ya baraza na walimu katika kuandaa mitihani ili kuhakikisha ubora na viwango vya kimataifa vinazingatiwa.

Nae, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Dk Mwanakhamis Adam Ameir, amesema baraza hilo  ni muhimili muhimu na hivyo linahitaji ushirikiano wa karibu na wataalamu ili kufanikisha majukumu lake ipasavyo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Baraza hilo, Othman Omar Othman, amesema watafanyia kazi maagizo yaliyotolewa  kwa maslahi ya baraza na taifa kwa ujumla.