AMIN Salum (30) mkazi wa mtaa wa Nyamarembo, Kata ya Mtakuja mjini Geita, ambaye ni mwendesha pikipiki ya abiria (bodaboda), ameuawa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Safia Shomary amethibitisha kutokea kwa tukio hilo wakati akizungumuza na waandishi wa habari na kueleza lilitokea Novemba mosi majira ya saa saba usiku.
Amesema watuhumiwa wa tukio hilo walikuwa kwenye harakati za kufanya uporaji kwa mkazi mmoja wa eneo hilo, ambapo hatua za uchunguzi zinaendelea kuwabaini wahusika.
“Ni tukio la kusikitisha, ambapo majambazi walikuwa wanataka kumpora mfanyabiashara mmoja ambaye jina lake linahifadhiwa na kwa bahati nzuri huyu mtu akakimbia baada ya kupata msaada wa bodaboda.
“Baada ya hapo wale bodaboda kwa kushirkiana na yule mhanga wakaanza kuwafukuza wale majambazi, kumbe wale majambazi walikuwa na silaha, wakamfyatulia yule bodaboda aliyekuwa anatoa msaada,” amesema.
Naye shuhuda wa tukio hilo, Wilihard Ulirick (29), ambaye alikuwa ni abiria wa marehemu amesema yeye na mwenzie walijitolea msaada wa kuwadhibiti wahalifu hao.
“Baada ya kutoa msaada huo wale jamaa (wahalifu) walikuwa na pikipiki wakakimbia, tukaamua tuwahi tukawadhibiti kwa mbele, mwenzagu akachukua pikipiki kwa haraka kabla wenye magari hawajafika tukawafuata.
“Tulipofika mbele tukaona kuna mwanga wa pikipiki, tukawaona hao raia nao wanapanda, tukawazibia njia, ghafla nilichosikia tu ni mlio wa risasi, sasa mimi mwenyewe tayari nikajikuta nimesharuka nikaanza kukimbia.
“Wakasimama wakataka kunifuata nikakimbia sana, kuna watu walikuwa wanakuja na magari ndio nikawasimamisha hapo, ikabidi tumfuate mwenzetu (bodaboda) kaelekea wapi, kumpigia simu haipokelewi, kumbe alikuwa ameshafariki.”
Mwendesha bodaboda wa mtaa wa Nyamarembo, Ibrahimu Chacha aliyekuwa anafanya kazi na marehemu katika kijiwe cha Msufini, amesema usiku wa tukio waliachana na Amin majira ya saa nne usiku wa Oktoba 31.
Amesema mnamo majira ya saa 11, alfajiri alipokea simu kujulishwa mwenzao Amin amefariki dunia kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana, taarifa ambayo ilimshitua, kwani marehemu hakuwahi kutoa taarifa ya ugomvi wowote.