Bodaboda kupewa elimu kupinga ukatili

MKUU wa Taasisi ya Ustawi wa Jamii, Dk Joyce Nyoni, amesema watatembelea madereva bodaboda katika vijiwe vyao, ili kuhakikisha elimu kuhusu kupinga ukatili imefanikiwa.

Dk  Nyoni  ameyasema hayo leo, wakati wa kufungua mafunzo kwa viongozi wa madereva bodaboda Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, ikiwa ni hatua ya kuelekea siku ya Ustawi wa Jamii Duniani Machi 21.

Amesema wanahitaji kuhakikisha vitendo vya ukatili vinaisha, kwani mtoto anaweza kafanyiwa ukatili akiwa mdogo na kuharibu uhusiano wake na maisha wakati wa ukubwani.

Amesema ukatili una madhara ya kisaikolojia, ambapo inaonkana kidonda kinapona lakini yale madhara ya kisaikolojia huwa hayaponi na hasa kama hajapata huduma stahiki kwa wakati.

“Tunaomba kama sehemu ya jamii kutokana na kazi zenu mnakutana na watu wengi mnabeba wadada, watoto ingawa wanasema watoto ni taifa la kesho sisi tunasema ni taifa la leo kwamba jinsi utakavyomlea leo ndio unavyotengeneza kizazi kijacho.

“Leo wewe ni kijana unanguvu kesho unakuwa mtu mzima je hiki kizazi kinachofuata huku nyuma unataka kiweje, sisi tunaona mna mchango mkubwa kuhakikisha jamii inastawi sawa sawa,” amesema.

Amewaambia viongozi hao wa madereva bodaboda wanawajengea uwezo wakienda sehemu zao za kazi, wawajengee uwezo wengine.

”Rais jana alisema tunapaswa kukemea vitendo vya kikatili sisi kama taifa kwa ujumla, tunaona tuna sehemu ya kufanya, niwaombe baada ya hapa mkawe mabalozi kuna vitendo vingi tunafanya na hatujui ni ukatili mfano dada anapita watu wanapiga miluzi ni ukatili atashindwa kujiamini,” amesema.

Habari Zifananazo

Back to top button