Bodaboda kusaidia vita ukatili wa kijinsia

VIJANA waendesha pikipiki za abiria (bodaboda) wilayani Geita wamesisitizwa kuwa mawakala wa haki na usawa wa kijinsia kwa kushiriki ulinzi wa mtoto wa kike na kupiga vita vitendo vya kikatili.

Kaimu Katibu Tawala wa Wilaya ya Geita, Janeth Mobe, amesema hayo wakati akihitimisha mashindano ya michezo kwa bodaboda yaliyoratibiwa na Mradi wa Kuwezesha Mabinti Balehe Kuendelea na Masomo (KAGIS).

Mradi wa KAGIS unatekelezwa na Shirika la Plan International kwa Ushirikiano na Shirika la Rafiki Develepment Organisation (RAFIKI SDO) kwa ufadhili wa Global Affairs Canada.

Amesema kupitia ushiriki wa waendesha bodabod,  serikali itaweza kufikia kusudio la kumsaidia mtoto wa kike aweze kusoma, asiweze kupata mimba za utotoni na asiweze kuolewa katika umri mdogo.

“Bodaboda tunawatumia kueneza hii kampeni, kwa sababu tunaamini watakuwa ndio walimu na mabalozi wetu kwa kuwa mara nyingi wanakutana na mabinti zetu na makundi tofauti,” amesema.

Ofisa Mradi wa KAGIS, Sabatho Simon amesema mashindano hayo yalizunduliwa mwezi Januari, 2023 kwa kukutanisha jumla ya timu 94 za waendesha bodaboda mkoani Geita.

Amesema kati ya timu washiriki, timu ya waendesha bodaboda ya Kata ya Ihanamilo wameibuka mabingwa wa mshindano ya KAGIS kwa kuifunga timu ya Kata ya Ludete kwa mabao 2-0.

“Tumeandaa mashindano na kuwaunganisha kwenye mradi waende wakawe mashujaa wa mabadiliko na kuwafundisha wenzao kuweza kufikia usawa na mabadiliko kwa mtoto,” amesema.

Amesema kupitia mashindano hayo ujumbe wa mradi wa KAGIS umeweza kufikia jamii kubwa kwa haraka zaidi, kwani michezo inakutanisha makundi ya watu wengi wa jinsi na jinsia tofauti.

Habari Zifananazo

Back to top button