Bodaboda Mara waandamana

walipa tano jeshi la Polisi

WASAFIRISHAJI wa abiria kwa kutumia Pikipiki maarufu  ‘Bodaboda’, wamefanya maandamano mjini Musoma, mkoani Mara kupongeza na kuunga mkono jitihada za Polisi katika kukabiliana na uhalifu.

Maandamano hayo yameanzia eneo la Musoma basi mpaka Kituo cha Polisi cha Wilaya hiyo kabla hayajapokewa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mara, Longnus Tibishubwamu nje ya ofisi yake.

Afisa Habari wa Umoja wa Bodaboda wa Mkoa huo, Faustine Mbarouk amesema wameona mabadiliko ya kiusalama, yanayotokana na jitihada zinazoongozwa na Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) Camillus Wambura, dhidi ya majambazi ambao wamekuwa wakijeruhi, wakiwachinja na kuwapora Pikipiki zako bila huruma.

“Tunaomba msikatishwe tamaa, muendelee kutusaidia kutulinda na sisi tunawaahidi ushirikiano,” amesema Mbarouk.

Amewataka vijana wenzake kuepuka kauli zinazotolewa na baadhi ya watu wakiwemo wanasiasa, ambazo licha ya kukwamisha vita dhidi ya uhalifu zinaweza kugeuzwa maficho ya wahalifu.

Naye Mwenyekiti wa Umoja wa Waendesha Bodaboda wa Manispaa ya Musoma, Stephano Silas, amesema wameandamana ili wenye nia ya kufanya uhalifu dhidi ya wananchi wa Mkoa huo wajue kwamba polisi hawapo peke yao bali wanao wadau ambao wanawaunga mkono na kusimama nao katika kuhakikisha usalama wa raia na mali zao unapatikana.

Bodaboda, wamefanya maandamano mjini Musoma,

“Majuzi tu dogo wetu Jose aliuliwa kwa kuchinjwa kinyama, bado tunashirikiana na polisi kupata wahusika, Bodaboda mmoja aliyejaribu kupora Pikipiki ya mwenzetu amehukumiwa kifungo jela, isingekuwa polisi kusimama haya mafanikio yasingepatikana,” amesema.

Naye RPC Tibishubwamu amewashukuru na kuwataka wendelee kuliunga mkono jeshi hilo huku akiwahakikishia kuwa lipo imara, wafanye kazi zao za usafirishaji wa abiria Saa 24 bila hofu yoyote.

 

Habari Zifananazo

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x