Bodaboda: tupo tayari kulipa kodi

KIGOMA UJIJI, Kigoma: MADEREVA pikipiki (bodaboda) na bajaji mkoani Kigoma wamesema kuwa wapo tayari kulipa kodi ya mapato kwa hiari kutokana na biashara ya usafirishaji wanayofanya wakiunga mkono mabadiliko ya Sheria ya Kodi iliyopitishwa na serikali mwaka 2023.

Waendesha bajaji hao na boda boda wametoa kauli hiyo wakati wa mkutano wa pamoja baina yao na maafisa wa Mamlaka ya Mapato (TRA) mkoa wa Kigoma. Mkutano uliokuwa ukitoa elimu na ufafanuzi wa sheria hiyo kwa madereva hao.

Mwenyekiti wa madereva boda boda Mkoa wa Kigoma, Samwel Mtema akizungumza katika mkutano huo amesema kuwa wamesikia uwepo wa mabadiliko ya sheria hiyo ya kodi iliyopitishwa na bunge na kwamba hawana pingamizi katika utekelezaji wa sheria hiyo.

Kwa upande wake Mussa Edson Mwenyekiti wa kijiwe cha boda boda, Nazareth Manispaa ya Kigoma Ujiji amesema kuwa Mkoa wa Kigoma umepiga hatua kubwa kwenye maendeleo ukiwemo ujenzi wa miundombinu ya barabara za lami ambayo msingi wake ni kodi inayokusanywa, hivyo kwa upande wao wamelipokea hilo ili kuunga mkono serikali katika ukusanyaji wa mapato yatakayogharamia shughuli za maendeleo ikiwemo kodi ya shilingi 65,000 wanayotakiwa kulipa kwa mwaka.

Akifungua mkutano huo Mkuu wa Wilaya Kigoma, Salum Kali amewataka waendesha pikipiki na bajaji kulichukulia suala la kulipa kodi kwa umakini kwakuwa serikali inajali uwepo wao kama wafanyabiashara lakini pia kama sehemu inayotoa ajira kubwa kwa watanzania.

Habari Zifananazo

Back to top button