Bodaboda wazidi kumkalia kooni Lema

CHAMA cha  Madereva na Wamiliki wa Pikipiki Tanzania (CHAMOPITA), Mkoa wa Tanga, kimemtaka Mwenyekiti wa CHADEMA, Kanda ya Kaskazini Godbless Lema kuwaomba radhi ndani ya siku saba kufuatia kauli  yake kuwa kazi ya bodaboda ni biashara iliyolaaniwa na pia haijarasimishwa.

Lema alitoa kauli hiyo hivi karibuni mkoani Arusha, wakati aliporejea nchini  kutoka Canada na kupokelewa na wafuasi wa chama chake.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Tanga, Mwenyekiti wa  CHAMOPITA, Michael Renatus amemtaka kiuongozi huyo wa kisiasa arudi kwenye vyombo vya habari, ili kukanusha kashfa hiyo kwa kundi la bodaboda nchini.

“Kitu ambacho kimetufanya tufike hapa  ni pale alipotoa kauli tata sasa sisi kama chama tunamtaka  arudi kwenye vyombo vya habari akakanushe kauli aliyoisema au atuombe radhi ndani ya siku saba, endapo hatafanya hivyo chama cha bodaboda kitafanya maandamano nchi nzima kupinga kauli za mwanasiasa huyo,”amesema Renatus.

“Kama sio kazi rasmi mbona bodaboda ndio ambao walimpokea kutoka uwanja wa ndege? Tumeumizwa na kauli zake ambazo zina lengo la kuleta uchonganishi kati yetu na serikali,” amesema.

Kwa upande wake muasisi wa bodaboda Wilaya ya Tanga mjini, Bakari  Masakuzi amelaani kauli hiyo kuwa ni ya ubaguzi, wakati kazi yao imekuwa  inawasaidia kwenye maisha ya kila siku.

Habari Zifananazo

Back to top button