Bodi mpya Ruwasa yapigwa msasa

NAIBU Waziri wa Maji, Mhandisi Maryprisca Mahundi ameitaka bodi ya pili ya wakurugenzi wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kufahamu na kusimamia viashiria hatarishi ili kuhakikisha ustawi na uendelevu wa taasisi hiyo.

“Wajumbe wa bodi mnahitaji kuwa na ufahamu wa viashiria hatarishi kwa taasisi ikiwa ni pamoja na kusimamia suala zima la maadili kwa watendaji kwani huo msingi muhimu wa uongozi bora na wenye tija kwa maendeleo endelevu,” alisema mjini Iringa wakati akifungua mafunzo kwa bodi hiyo yenye wajumbe 13.

Mhandisi Mahundi amekiri kuwepo na changamoto ya upungufu wa bajeti ya Ruwasa lakini pia changamoto ya uharibifu wa vyanzo vya maji hali inayopelekea kukauka kwa mito na kukosekana kwa maji.

Advertisement

Akizungumzia umuhimu wa mafunzo hayo kwa bodi hiyo alisema yatawasaidia kutekeleza majukumu yao ya kibodi kwa weledi na ufanisi utakaowezesha Ruwasa kufanya kazi zake kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu.

“Kwahiyo watapitishwa kuijua taasisi yao na dhamana ya bodi. Watafundishwa misingi ya usimamizi wa taasisi za umma, dhana ya utawala bora, na majukumu ya bodi na menejimenti,” alisema.

Aidha Mhandisi Mahundi ameeleza kufurahishwa na kasi ya utekelezaji wa miradi ya maji nchini inayofanywa na RUWASA akisema inatafsiri kwa vitendo dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan inayolenga kuhakikisha huduma hiyo inapatikana katika vijiji vyote nchini kama ilivyo mijini.

Mhandisi Mahundi ambae alimwakilisha waziri wa Maji Jumaa Awesso alisema Wizara inajivunia utendaji kazi wa Ruwasa

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Ruwasa, Bwai Biseko alisema bodi hiyo mpya inalo jukumu la kusimamia shughuli za taasisi hiyo kupitia mpango mkakati wao wa mwaka 2019/2020 hadi 2024/2025.

“Tunawapa mafunzo kwasababu ni muhimu wailewe taasisi wanayoiongoza kwa mujibu wa sera na sheria ya maji Na 19 ya mwaka 2019 na shughuli zake ikiwemo ujenzi wa miradi ya maji na usimamizi wa utoaji wa huduma ya maji,” alisema.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Ruwasa Mhandisi Ruth Koya alimshukuru Rais kwa kumteua kuwa Mwenyekiti wa bodi ya pili ya RUWASA akisema ataifanya kazi hiyo kwa weledi ili kuiwezesha RUWASA kufikia malengo yake katika ujenzi wa miradi ya maji nchini.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *