Bodi PURA yapongeza utendaji GASCO
BODI ya Wakurungezi ya mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA), imepongeza kampuni tanzu (GASCO) ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Nchini (TPDC), kwa kuendesha kwa ufanisi mitambo ya kuchakata gesi asilia iliyopo eneo la Madimba, mkoani Mtwara.
Bodi hiyo imeambatana na wajumbe wa kamati za bodi, menejimenti ya PURA, na baadhi ya wataalamu kutoka PURA, wamefanya ziara ya kutembelea mitambo hiyo ya kuchakata gesi asilia na visima vya kuzalisha gesi vilivyopo Mnazi bay Mkoani Mtwara, kwa lengo la kuongeza uelewa wa shughuli zinazotekelezwa na mamlaka hiyo ya PURA.
“Tumefarajika kwa kweli kuona kwamba mtambo huu unaendeshwa na Watanzania watupu, unaendeshwa vizuri sana na kwa ufanisi zaidi na haujachakaa,” amesema Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurungezi, Beng’i Issa.
Kufuatia hatua hiyo, Beng’i ameshauri serikali kuendelea kuiwezesha TPDC kwa kuijengea uwezo zaidi, ili iweze kufanya miradi mingine mikubwa, ikiwemo mradi wa LNG ambao unatarajiwa kuanza kujengwa mkoani Lindi.
“Ninachopenda kusema ni kutoa rai yangu kwa serikali yetu, iangalie taasisi hizi Kama TPDC na PURA kwa kuziwezesha vizuri, ili kusudi ziweze kuendeleza sekta ya gesi asilia na mafuta kwa umuhimu wake,” amesema.
Meneja anayesimamia shughuli za uendeshaji kwenye mitambo ya kuchakata gesi ya Madimba, Mhandisi Sultan Pwaga, amesema wanajivunia kuona Watanzania wanaendesha mitambo hiyo kwa ufanisi pamoja na matengenezo yake na kuweza kuzalisha gesi.
“Swala kubwa la kujivunia tokea Watanzania tupewe dhamana hii takribani miaka mitano sasa, tumeweza kuendesha mitambo hii kwa ufanisi mkubwa pamoja na matengenezo yake,” amesema.
Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Halfani Halfani amesema kuwa ziara hiyo imekuwa na manufaa makubwa, hususani kwa wajumbe wapya na kamati za bodi walioteuliwa hivi karibuni, ambao hawakuwa wamefika maeneo hayo.