Bodi ya Wakurugenzi Ngorongoro, watembelea Ifisi
BODI ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro ( NCAA) ikiongozwa na Mwenyekiti wake Jenerali Venance Mabeyo ( Mstaafu) wametembelea Bustani ya Wanyamapori iliyopo katika eneo la Ifisi Jijini Mbeya ambapo katika ziara hiyo wamefurahishwa na uwekezaji uliofanywa.
Bodi hiyo pia ilipata fursa ya kutembelea moja ya Makumbusho ya urithi wa utamaduni ambayo imesheheni mikusanyo ya aina mbalimbali ya makabila ya Nyanda za Juu Kusini ambayo ina inavifaa vya waganga wa jadi vya kishirikina ambayo ni sehemu ya utamaduni wa watu wa Nyanda hizo.
Wakati wa ziara hiyo Mwenyekiti Mabeyo amefurahishwa na jitihada za Mkurugenzi Mshauri wa Kanisa la Uinjilisiti ambaye ni Muanzilishi wa Bustani ya wanyamapori hai, Markus Lehner kwa usimamizi mzuri wa kulifanya eneo hilo kuwa la kipekee na lenye mvuto wa namna yake kwa watalii
Kufuatia hatua hiyo ya uwekezaji, Mwenyekiti huyo ametoa pongezi kwa Uongozi wa Bustani hiyo kwa hatua ilizozichukua za kuhifadhi na kuenzi utamaduni wa watu wa Nyanda za Juu Kusini kwa kufungua Makumbusho hiyo ambayo mbali ya kuwa kivutio cha utalii lakini pia ni kioo cha kujitazama kama Taifa tumetoka wapi na tunaelekea wapi .
Amesema ni wakati sasa wa Taasisi na watu binafsi kufungua Makumbusho nyinginezo kwa lengo la kuhifadhi na kuenzi utamaduni wetu kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mshauri wa Kanisa la Uinjilisiti ambaye ni Muanzilishi wa Bustani ya wanyamapori hai, Markus Lehner amewaeleza Wakurugenzi wa Bodi hiyo kuwa anapenda Uhifadhi wa wanyamapori huku akisisitiza kuwa amekuwa akitumia muda mwingi kuhakikisha miundombinu ya utalii inaboreshwa ili kuwafanya watalii wanapotembelea eneo hilo wanafurahia na wanakuwa Mabalozi wazuri kwa watalii wengine.
Nina wanyama wa kila aina wakiwemo simba, chatu, nyumbu pamoja ndege mbalimbali ili kuhakikisha uwekezaji huu unakuwa endelevu nimesomesha vijana wenyeji wa maeneo haya ambao ndio wamekuwa nguzo ya kuhakikisha kila kitu kinakwenda sawa” amesisitiza
Lengo kuu la ziara hiyo ni kujifunza ikiwa ni Mkakati wa Bodi hiyo kuhakikisha NCAA inafungua Bustani ya Wanyamapori katika eneo la Kimondo cha Mbozi ili watalii wakifika katika eneo hilo wakute vitu vingi vya kutembelea.
Bustani hiyo ya wanyama hai pamoja na Makumbusho hiyo imekuwa ikiwavutia watalii wengu kutembelea kwa vile ni eneo ambalo Watalii hutumia muda mwingi wa kuona vivutio vingi vya utalii kwa wakati mmoja.