Bodi yaanza kampeni urejeshaji mito

BODI ya Maji Bonde la Wami Ruvu imeanzisha kampeni maalumu ya urejeshaji wa mito mitano iliyopoteza uelekeo kwenye asili yake ambayo  vyanzo vyake vya  maji  vinatoka kwenye safu ya milima ya Uluguru.

Mito hiyo ni Mlali, Mgera, Lukulunge, Ngerengere na Mzinga inapatikana katika wilaya ya Mvomero na Morogoro na kupoteza uelekeo kwenye asili yake kumechangiwa na shughuli za kibinadamu  kando ya mito hiyo hivyo kuchangia uharibifu wa mazingira.

Ofisa Rasilimali Maji wa Bodi ya Maji Bonde hilo, Martin Kasambala  alisema hayo kwenye  taarifa ya  mradi wa upandaji wa miti  eneo la Bwawa la Mindu katika Manispaa ya Morogoro  kwa Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru 2023 Kitaifa, Abdalla Shaib Kaim .

Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru na timu yake walishiriki na wananchi katika zoezi la upandaji miti eneo la bwawa hilo ambalo limezungukwa na kata nne  ya  Mindu, Luhungo, Magadu na Kauzeni.

Kasambala amesema katika kutekeleza kampeni hiyo   jumla ya miti 15,500 imeshapandwa kwenye chanzo cha Bwawa  hilo na lengo ni kupanda miti 200,000 kwa mwaka katika maeneo  yanayosimamiwa na Bonde la Wami Ruvu.

“ Tumeanzisha kitalu cha miche ya miti ya aina mbalimbali ikiwemo matunda chenye idadi ya miti 30,800 ikiwa ni hatua za awali sambamba na kusafisha mito hiyo ili kuwezesha mikondo yake ya asili iweza kurejea kama hapo awali ” amesema Kasambala

Kasambala amesema  kuwa Bwawa la Mindu ni miongoni mwa vyanzo 231 vya maji vinavyosimamiwa na Bodi ya maji ya Bonde la Wami  Ruvu  na linategemewa  kwa asilimia 75  ya wakazi wa Manispaa ya Morogoro.

Alisema  Bodi ya Bonde hilo imeanza  kutekeleza Agizo la Makamu wa Rais, Dk  Philipo Isidory Mpango la kupanda miti  laki mbili  kwa kila Mkoa alilolitoa Novemba 2022 mkoani Mbeya wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Mwaka wa Bodi za Maji za Mabonde.

Kasambala amesema kwenye utekelezaji wa kampeni hiyo zitanatajiwa kutumika sh milioni 50 kwa usambazaji wa miti,nguvu kazi itakayotumika na masuala mengine ya ulinzi na uhifadhi wa vyanzo vya maji.

Ametaja hatua nyingine ni utoaji wa elimu kwa jamii juu utunzaji na uhifadhi wa vyanzo vya maji , kusimika mabango 100 ya makatazo kwenye vyanzo vya maji,  usimikaji wa alama za kudumu za mipaka (beacon) zaidi ya 1,000 pembezoni mwa vyanzo vya maji.

Kwa upande wake kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru 2023 Kitaifa , Kaim , amewaasa wananchi  kuacha kufanya shughuli za kibinadamu karibu na maeneo ya vyanzo bya maji ili kuruhusu uendelevu wamaji .

“ Kupotea kwa uoto wa asili ni matokeo ya kufanya  shughuli za kibinadamu kwenye hifadhi za misitu na vyanzo vya maji kinyume na miongozo ya kisheria hivyo ni vyema wananchi wakaacha tabia hii” amesema  Kaim

Amesema serikali inaendelea  na mkakati wa kukabiliana  na mabadiliko ya tabianchi kwa uhamasishaji wa upandaji miti , kuhifadhi  mazingira na kutunza vyanzo vya maji .

Hivyo ameipongeza Bodi ya Maji Bonde la Wami Ruvu kwa kutii agizo  la serikali lililotolewa na Makamu wa Rais  ikielekeza Bodi zote za maji kupanda miti zaidi ya 2,000,000.

Habari Zifananazo

Back to top button