Bodi kuleta bei shindani ya mazao

BODI ya Usimamizi wa Stakabadhi Ghalani nchini imeeleza mfumo wa stakabadhi hauna lengo la kupandisha bei wala kupunguza katika ununuzi wa mazao bali ni kuleta bei shindani katika soko la mazao.

Mkurugenzi wa bodi hiyo, Asangye Bangu ameeleza hayo Februari 14, 2024 katika kikao cha wadau wa stakabadhi ghalani ambapo alisema ni vizuri kuratibu ujenzi wa maghala kwa mkoa huu ambao umeonekana kuwa na maghala mengi yaliyo chakaa.

“Mkoa umedhamiria stakabadhi ghalani mambo mengi yana tafsiriwa na wananchi wengi wanajishughulisha na masuala ya kilimo mfumo wa stakabadhi unakubali maoni, michango na maboresho na umeletwa ili kuondoa mawazo hasi yaliyopo”alisema Bangu.

Ofisa biashara kutoka bodi hiyo akiwasilisha taarifa mbele ya wadau alisema tayari mazao 14 yamekwisha jiunga katika mfumo huo ikiwa baadhi ya ushirika umeanza kufanya mchakato wa kuingiza mazao.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Christina Mndeme ambaye alikuwa mgeni rasmi katika kikao hicho alisema hakuna anayepinga mfumo na wote waliukubali na kuhakikisha utafanyiwa kazi nakuondoa changamoto zilizokuwepo.

Mndeme alisema mfumo huu unasaidia wakulima kupata taarifa na takwimu mbalimbali za mazao kwa wakati na usahihi ikiwa kabla ya uwepo mfumo huu ilikuwa ni ngumu kupata taarifa pamoja na takwimu za mazao kwa wakati sahihi.

“Mkulima asicheleweshewe fedha zake kusiwepo changamoto ya mfumo alipwe Kama ilivyokubalika na mnavyoeleza ni kwa muda wa siku tatu.”alisema Mndeme.

Mjumbe wa Bodi ya Chama Kikuu cha Ushirika mkoani Shinyanga (Shirecu) Charles Gishuli alisema mfumo huu sio wa ushirika bali ni utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambapo ushirika unatekeleza na ulianza katika mazao ya mikunde na wamefanya vizuri zaidi.

Mwenyekiti wa wafanyabiashara wa mazao ya dengu na kunde, Hassan Mboje alisema kinachokwamishwa ni bei na tozo kubwa ndiyo maana mwaka wa sita sasa mfumo unatangazwa na kupotea.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Mabala Mlolwa alisema wanaoenda kusimamia mfumo huu wawe wazalendo na maelezo ya mkulima kulipwa siku tatu yawe ya uhakika.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Ngasa Mboje alisema tozo hazitamhusu mkulima kwa wakulima wa choroko na dengu kwani kupitia mfumo huu mwaka 2021 walikusanya mazao yakawa ghalani yakakosa mnunuzi hivyo taasisi za fedha wanatakiwa kusema ukweli.

Habari Zifananazo

Back to top button