BODI ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB),imeupongeza uongozi wa kampuni hodhi ya Mkulazi kwa kufuata sheria na kanuni za bodi hiyo kwenye ujenzi majengo mbalimbali ya kiwanda hicho cha kuzalisha sukari nchini.
Ofisa Uhusiano wa Bodi hiyo , Atugonza Samwel amesema hayo wakati wa ziara ya kutembelea mradi wa kiwanda kinachozalisha sukari kilichopo Mbigiri kata ya Dumila, Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro.
Atugonza amesema bodi imeweka mpango endelevu wa kutembelea miradi mbalimbali nchini kwa lengo la kukagua na kufanya tathimini ya ufuatiliaji wa majengo .
Amesema zoezi hilo litasaidia wawekezaji wote nchini kuweza kutumia wabunifu wa majengo na wakadiriaji majenzi ili kuweza kuwa na majengo bora ambayo hayataweza kusababisha madhara yoyote kwa wananchi wa Tanzania.
“Tumekitembelea kiwanda hiki kwenye maeneo yake mbalimbali, sehemu za makazi ya wafanyakazi wa kiwanda , Zahanati ya Kiwanda na eneo la kiwandas chenyewe za uzalishaji wa sukari mimi nikiwa mfanyakazi wa AQRB kwa kweli nimeridhika. “ amesema Atugonza .
Ametoa wito kwa Watanzania wanapotaka kuwekeza katika miradi mbalimbali ya biashara, viwanda na nyumba za makazi kabla ya kujenga ni vyema kuzingatia sheria na kanuni za majenzi zilizotolewa na AQRB kwa kupata ushauri na kutumia wataalamu waliosajiliwa na bodi.
“ Ni vyema watanzania tukazingatia kanuni na sheria hizi ,kwani zisipofuatwa tutajikuta kwenye sehemu za kuleta madhara mabaya kwa wananchi kwa mfano jengo linaweza kuporomoka ghafla na tunaweza kusababaisha vifo kwa wananchi wetu. “ amesema Atugonza.
Naye Mkuu wa Idara ya Miliki ya Kampuni Hodhi ya Mkulazi, Mhandisi Jacob Swere amesema mafanikio makubwa ya ubora wa majengo mbalimbali yaliyopo kwenye Kiwanda hicho kumechangiwa na kuwatumia wataalamu ambao wamesajiliwa na AQRB.
“Bodi hii imekuwa ikitusimamia vizuri hata kwenye maeneo yale ambayo ni miongozo mizuri katika majenzi yetu hasa tunapozungumzia watu wenye mahitaji maalumu na masuala ya kiusalama yakiwem ya kujikinga na moto “ amesema.” Mhandisi Swere.
Mhandisi Swere amesema uongozi wa kampuni umezingatia na kufuata viwango vilivyotakiwa kufuatwa kwenye majenzi katika majengo yote ya kiwanda kuanzia nyumba za wafanyakazi, ofisi, zahanati hadi majengo ya kiwandani ( kwenye uzalishaji) yamezingatia mahitaji yote wakiwemo ya watu wenye mahitaji maalumu.
Kwa upande wake ofisa uhusiano wa kampuni hiyo , Clemetina Patrick ameishukuru AQRB wa kutoa ushirikiano wa ukaguzi wa ujenzi wa kiwanda hicho ni kipya sukari cha Mkulazi ambacho kwa sasa kimeanza uzalishaji wake na kutoa sukari yake ya kwanza.