Bodi za Usajili wa Wahandisi Tanzania, Kenya zashirikiana

BODI ya Usajili wa Wahandisi Tanzania (ERB) imeahidi kuendeleza ushirikiano na Bodi ya Usajili wa Wahandisi ya Kenya (EBK) kupitia mkataba wa makubaliano ya pamoja waliyoweka ili kuhakikisha wanakidhi vigezo vya ushindani katika nchi za Umoja wa Afrika Mashariki (EAC) na dunia kwa ujumla.

Akizungumza wakati wa kufunga warsha ya wiki moja iliyoandaliwa na ERB jijini hapa, Msajili wa Bodi hiyo, Benard Kavishe alisema dhumuni la warsha hiyo ni kuboresha mazingira ya kutambulika wahandisi wa taaluma hiyo.

Taaluma hiyo itasaidia mhandisi kutoka Tanzania, Kenya pamoja na wale walio katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kutambulika na kufanya kazi katika nchi hizo bila ya vizuizi vyovyote.

Advertisement

“Haya ni makubaliano ambayo tuliafikiana tangu mwaka 2012, lengo likiwa ni kuwasaidia wahandisi waliosajiliwa katika nchi hizi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kuweza kufanya shuguli zao bila vizuizi. Pia kukutana na kubadilishana uzoefu wa kitaalamu ili wote kuwa na viwango vinavyofanana,” alisema.

Tangu makubaliano hayo kuafikiwa kumekuwa na ziara na warsha za mara kwa mara kwa wahandisi hao ambapo kwa mwaka huu warsha ya kujengea uwezo wataalamu hao imefanyika jijini hapa.

Alitaja baadhi ya vigezo vilivyomo katika makubaliano yao ni pamoja na kuwa na viwango sawa katika ufundishaji, usajili na kuwalea katika hali itakayorahisisha utendaji kazi na kufungua ajira katika nchi za Afrika Mashariki.

“Tulipokea ugeni wa watu tisa kutoka Kenya ambao wamekuja kujifunza na kubadilishana uzoefu, tulichukua kutoka kwao kile ambacho hatuna na kile ambacho hawana wamechukua kutoka kwetu,” alisema.

Baada ya ziara hiyo kumalizika, anaamini kuwa wahandisi wa Tanzania na Kenya watafanana katika viwango vyao vya kiutendaji na hivyo kuendeleza ushirikiano na kuwa na ushindani dunia nzima.

Kwa upande wake, Mhandisi wa Bodi ya Usajili ya Kenya (EBK), Margaret Ogai alisema kupitia warsha hiyo wamejifunza mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja utaratibu wa kufanya mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi wanaotoka vyuoni waliosoma taaluma ya kihandisi.

Margaret alisema pia wamejifunza kwenda kuanzisha mfuko maalumu kwa ajili ya kusaidia wahandisi kupata mafunzo ya kuwajengea uwezo na kusajili wahandisi wengi wa kike wa chini ya miaka 35.

Naye, Mhandisi mwingine kutoka Kenya, Monica Wangari alisema warsha hiyo imesaidia kujua masuala mengi ambayo anaamini kwa namna moja ama nyingine yataenda kufungua fursa ya ajira kwa wahandisi wengi wa Tanzania na Kenya pamoja na wale walio katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Alipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa maendeleo yaliyofanyika katika Jiji la Dodoma ambapo licha ya mafunzo waliopata katika warsha hiyo, pia walipata fursa ya kutembelea mji wa serikali eneo la Mtumba na kuona namna ulivyopangika na kuvutia.

Veronica Ninalo kutoka ERB, ambaye ni mshiriki kutoka Tanzania aliomba Serikali ya Tanzania kupitia bodi hiyo kuandaa warsha za mara kwa mara ili kubadilishana uzoefu kutoka sehemu mbalimbali ili kuimarisha na kuboresha taaluma hiyo.