UJENZI wa bomba la kusafirisha gesi asilia kutoka Ntorya kwenda Kiwanda cha uchakataji cha Madimba mkoani Mtwara linatarajia kuanza muda wowote kuanzia sasa.
Hatua hiyo imetajwa baada ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Nchin (TPDC) kukamilisha malipo ya fidia kwa wakazi 225 ambao maeneo yao yamechukuliwa kwa ajili ya ujenzi wa bomba hilo.
Afisa Uhusiano na Mawasiliano TPDC Jacob Haule amesema hayo leo katika zoezi la kukamilisha ulipaji wa fidia kwa wananchi 19 ambao walikuwa wamesalia.
“Leo tupo hapa Mtwara Kijiji cha Mtendachi Madimba Mkoani Mtwara kukamilisha zoezi la ulipaji wa fidia kwa wananchi ambao wanatarajia kupisha mradi wa ujenzi wa Bomba la Gesi kutoka Ntorya kwenda Madimba,” amesema.
Haule amesema kwamba mara baada ya kukamilika kwa zoezi la ulipaji wa fidia, ujenzi utaanza muda wowote kuanzia sasa.
“Tunatarajia mradi uanze kutekelezwa kwa haraka kwa sababu ni mradi muhimu na lengo hasa ni kuongeza kiwango cha gesi katika bomba kubwa ambalo linasafirisha Gesi kwenda Dar es Salaam,” amesema.
Katika hatua nyingine, Haule amesema takribani wananchi 255 katika vijiji 11 na kata tano wametoa sehemu ya maeneo yao kupisha utekelezaji wa mradi huo.
Haule amesema zaidi ya shilingi milioni 430 zimetumika kulipa fidia kwa wananchi wanaopisha mradi huo.
Gesi asilia inatumika nchini kwa ajili ya kuzalisha umeme, kupikia majumbani, kwenye magari na viwandani.
Zaidi ya asilimia 70 ya umeme unaotumika nchini unatokana gesi asilia.