Bongozozo atangaza utalii Kusini

BALOZI wa hiari wa kutangaza utalii wa Kusini mwa Tanzania, Nicholas Reynolds maarufa kama Bongozozo amesema baada ya kufanya ziara katika vivutio sita ameweza kuchukua video na kusambaza katika mitandao ya kijamii, ili kuvutia watalii wa nje ya nchi.

Bongozozo alifanya ziara kwa siku 13 kuanzia Juni 12 hadi Juni 24,2023 katika mikoa ya Kusini lengo likiwa ni kutangaza utalii kwa ukanda huo.

Amesema katika ziara hiyo amerekodi video katika maeneo mbalimbali, ili kusambaza katika akaunti zake za mitandao ya kijamii, ikiwemo Tiktok, ambayo ipo kwa lugha ya Kiingereza na kufanya watu wengi kufahamu kuhusu vivutio hivyo.

Advertisement

“Tulienda kwenye maporomoko tukatengenza video nzuri na tuliogelea na maporomoko mengine mazuri zaidi kila maporomoko yana sifa yake nzuri kulikuwa na maporomoko 14  na nilienda na mtaalamu wa mtandao wa Tiktok na tuliweza kufikisha habari katika mitandao ya kijamii ,”ameeleza Bongozozo.

Vivutio vilivyotembelewa ni pamoja na Hifadhi za Taifa za Milima Udzungwa, Ruaha na Nyerere, pori la akiba la Mpanga Kipengere,kikundi cha Utalii wa Kitamaduni –Mtera Izazi na Hifadhi ya Urithi wa Utamaduni wa Dunia Mgofu ya Kilwa Kisiwani na Songo Mnara.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu  wa TTB, Damasi Mfugale amesema lengo la ziara hiyo ya mafunzo ni kutangaza vivutio vya utalii vinavyopatikana Kusini mwa Tanzania, ili kuongeza ufahamu na kuongeza idadi ya watalii.

“Pia kuleta ushawishi kwa Watanzania kutembela vivutio hivyo, ambapo TTB ilifanya ubia na kampuni kutoka Kusini ambazo waliweza kuuza vifurushi na kuleta watalii, ili kutalii na Bongozozo ikiwemo na vifurushi hivyo vilileta Watanzania 63 na Muingereza Mmoja waliotembelea Milima Udzungwa,Ruaha na Nyerere na pori la akiba la Mpanga Kipengere ,”ameeleza Mfugale.

Alibainisha kuwa bodi ya utalii ipo kwenye utekelezaji wa mikakati miwili wa utangazaji utalii wa kusini mwa Tanzania mpango wa mwaka 2021-2026, ambapo iliandaliwa kupia mradi wa REGROW na kuzinduliwa Mwezi Septemba ,2022 mkoani Njombe.

Amesema mikakati hiyo imetaja njia mbalimbali za utangazaji wa utalii ikiwa ni pamoja na kutumia watu maarufa/mabalozi wa hiari,utagazaji kwa njia ya mtandao ,vyombo vya habari ,ziara ya mafunzo na kushiriki katika maonesho ya kibiashara.

/* */