DAR ES SALAAM; MKURUGENZI Mtendaji wa Kampuni ya Kalito’s Way Group, Carlos Kalito, amesema wameaajiri Watanzania 500 na kwamba mafanikio ya biashara yake ya migahawa nchini Tanzania inatokana na ubunifu uvumbuzi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa sherehe za maadhimisho ya miaka 17, zilizopewa jina la “Hatushkiki Tunaua Kila Siku,” Kalito, anayemiliki migahawa ya Samaki Samaki, Kuku Kuku na Wavuvi Camp, amesema pia mazingira mazuri ya uwekezaji nchini ni sababu kuu ya mafanikio yao.
Alisema kuwa tangu kuanzishwa kwao mwaka 2007, kampuni imekua kwa kiasi kikubwa, kama inavyoonekana kwenye ongezeko la idadi ya wafanyakazi wao.
Kwa mujibu wa Kalito, biashara ya vyakula vya baharini (seafoods) na vinywaji inahitaji kiwango cha juu cha ubunifu na uvumbuzi, ili kushindana na wengine.
“Nina fahari kuchangia soko la ajira licha ya changamoto, hasa ushindani wa soko. Tuna watu wabunifu, ambao wametusaidia kufikia mafanikio haya, na tunaendelea kusonga mbele.
“Tuna matawi kadhaa jijini ambayo yanafanya vizuri. Ili kuhakikisha tunadumisha nafasi yetu sokoni, tumeamua kusherehekea maadhimisho yetu ya miaka 17 kwa mbwembwe,” amesema Kalito.
Kama sehemu ya sherehe, kampuni imeanzisha promosheni ya “Hatushikiki Tunaua Kila Siku,” inayotoa wateja fursa ya kupata aina mbalimbali za vyakula na burudani.
Kalito amesema kuwa wasanii mbalimbali watatumbuiza katika tawi lao la Mlimani City, Wavuvi Camp, na maeneo mengine ili kuwapa wateja burudani wanayopenda.
Meneja wa burudani wa kundi hilo, Hellen Kazimoto, alisema wamepanga kutoa burudani ya kipekee.
“Kampeni ya Hatushkiki ni ya kipekee, na tutatoa fursa kwa wasanii mbalimbali wa ndani. Kila siku tutakuwa na burudani tofauti, zote bila mipaka ya muda,” amesema.