BoT kuhuisha Mfuko wa Dhamana uuzaji bidhaa nje
WIZARA ya Fedha na Mipango imesema serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT) itahuisha Mfuko wa Dhamana kwa wakopaji wanaozalisha bidhaa za kuuza nje ya nchi ili kuongeza uzalishaji.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba amesema katika kutekeleza mkakati huo, Sh bilioni 600 zinatarajiwa kutumika; na BoT itatoa Sh bilioni 280 na Benki ya Dunia itatoa mkopo nafuu wa dola za Marekani milioni 150.
“Hatua hii itawezesha uzalishaji na kuongeza mauzo ya bidhaa zetu nje ya nchi,” alisema Dk Mwigulu wakati akiwasilisha Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 bungeni jijini hapa juzi.
Alisema serikali imeamua kuchukua hatua mahususi za muda mfupi, wa kati na mrefu kuimarisha sekta ya uzalishaji. Alitaja miongoni mwa hatua hizo ni mkakati wa kuongeza uzalishaji ili kuongeza mauzo ya bidhaa zetu nje ya nchi na kupunguza uagizaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi.
Alisema serikali itaendelea kushirikiana kwa karibu na wazalishaji wa mazao ya kilimo, mifugo, uvuvi na viwanda vinavyoongeza thamani na kuzalisha bidhaa ili kuhakikisha kuwa tunaongeza tija katika uzalishaji wetu.
Dk Mwigulu alisema jawabu la ukosefu wa ajira kwa vijana na kuondoa umasikini kwa Watanzania ni kukuza uwekezaji hususani katika sekta za uzalishaji na kuimarisha ushiriki wa sekta binafsi.
Alisema maono ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuimarisha ushiriki wa sekta binafsi ni sahihi na kwa wakati sahihi. Dk Mwigulu aliagiza watendaji serikalini wawe na nidhamu ya kuilea na kuiwezesha sekta binafsi kukua na kushiriki kikamilifu katika kukuza uchumi.
“Tunatumia nguvu kubwa sana kwenye kudhibiti kuliko nguvu tunayoitumia kuwezesha. Lazima tuheshimu sekta binafsi na kutambua mchango wake katika kutoa ajira, kuondoa umaskini na kukuza uchumi. Nitoe rai kwa Watanzania wenzangu tuwe na nidhamu katika kuiwezesha sekta binafsi kukua,” alisema Dk Mwigulu.
Alisema serikali inaendelea kutekeleza Sera za Fedha na Mpango wa Serikali wa Kuboresha Mazingira ya Biashara.
Alisema utekelezaji wa sera hizo umewezesha kushuka kwa viwango vya riba za mikopo ya benki na katika kipindi cha mwaka kinachoishia Aprili mwaka huu viwango vya riba za mikopo vilipungua na kufikia wastani wa asilimia 15.
91 kutoka wastani wa asilimia 16.58 Aprili 2021. Kupungua kwa viwango vya riba za mikopo kumeelezwa kumechangia kuongezeka kwa mikopo kwa sekta binafsi ambako mikopo hiyo imeongezeka kwa asilimia 22.
5 Aprili 2023 ikilinganishwa na asilimia 4.8 Aprili 2021