BRELA itambue miliki bunifu -Mwana FA

DAR ES SALAAM: SERIKALI imeielekeza Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) kuwatambua wabunifu na kuhakikisha wanapata dhamana zinazowawezesha kukopesheka Ili kunufaika na ubunifu wao.

Naibu Waziri wa Utamaduni ,Sanaa na Michezo Hamisi Mwinjuma amesema hayo leo Dar es Salaam katika maadhimisho ya siku ya miliki ubunifu duniani.

Amesema kwa kufanya hivyo itawezesha miliki bunifu kuondoa changamoto na kuongeza kipato cha mtu mmoja mmoja nchini.

“Wapo wabunifu wengi nchini ambao ubunifu wao hawajanufaika nao,hivyo Kwa kuwatambua itasaidia kupata mikopo kutoka benki mbalimbali ambayo wataitumia kujiendeleza na kunufaika zaidi,” amesema.

Amesema Kwa upande wa serikali itahakikisha kuweka mazingira na sera imara katika kuimarisha miliki bunifu nchini.

Amesema maendeleo ya nchi yanategemea miliki bunifu kwa ukuaji wa uchumi.

“Serikali ina uhakika kuwa miliki bunifu zitaondoa changamoto kwa jamii na zitaongeza ukuaji wa uchumi Kwa mtu mmoja mmoja,”amesema Mwinjuma.

Mwinjumaa amesema anatambua kazi nzuri inayofanywa na BRELA katika kuwaimarisha wafanyabiashara na wenye makampuni kutekeleza shughuli zao za kimaendeleo.

“Tutahakikisha ifikapo mwaka 2030 kunakuwa na uwiano wa maendeleo duniani kwa kutumia miliki bunifu”,amesema

Amesema Serikali kwa kushirikiana na Taasisi nyingine itawezesha ukamilikaji wa sera ya miliki bunifu ambayo italeta mwanga katika kusimamia mwongozo wa hati miliki Tanzania.

Aidha aliitaka BRELA kuelekea Maadhimisho hayo yatumike kama fursa ya kujadili na yatolewe maoni yatakayofanyiwa kazi.

Isome pia https://habarileo.co.tz/53362-2/

Naye, Ofisa Mtendaji Mkuu wa BRELA Godfrey Nyaisa amesema masuala ya ubunifu yatasaidia kusukuma gurudumu la maendeleo mbele.

Amesema hivi sasa wana mpango wa kuanzisha programu ya miliki bunifu katika vyuo vyote nchini lengo ni kuendeleza ubunifu nchini.

Nyaisa amesema nchi nyingi zinaendelea duniani kwa sababu ya kueneza miliki bunifu sehemu mbalimbali ndani ya nchi zao.

Naye Mwenyekiti wa bodi ya ushauri BRELA Profesa Neema Mori amesema maadhimisho hayo ni muhimu kuendelea kusheherekewa nchini kwani yanatoa fursa ya kukutanisha wadau mbalimbali na kuweza kujadiliana,kujifunza na kupata fursa ambazo zitasaidia kukuza bunifu za wabunifu nchini.

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button