Brela yajadili namna kukuza uchumi
WAKALA wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), umesema ili kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji nchini ni vyema kujadili kwa pamoja vikwazo vinavyosababishwa na usimamizi wa sheria, kanuni na taratibu zinazotumika na kuangalia jinsi ya kuvikwamua, ili kukuza uchumi wa Tanzania.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Godfrey Nyaisa alisema hayo mjini Morogoro katika hotuba yake ya ufunguzi wa kikao kazi kati ya wakala huo na taaisisi za udhibiti wakiwemo wanasheria na maofisa wanaohusika na utoaji wa vibali mbalimbali.
Kikao kazi hicho kililenga kujadili mikakati ya pamoja ya namna ya kutatua mikinzano inayojitokeza katika utendaji kazi wa kila siku.
Nyaisa alisema ili kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji nchini ni vyema kujadili kwa pamoja vikwazo vinavyosababishwa na usimamizi wa sheria, kanuni na taratibu zinazotumika na kuangalia jinsi ya kuvikwamua, ili kukuza uchumi wa Tanzania.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa BRELA alisema serikali imedhamiria kuinua hali ya uchumi wa nchi.
“ Hivyo BRELA katika kuunga mkono jitihada hizo, inakutana nanyi ili kujadili mikinzano na muingiliano katika utoaji wa huduma na jinsi ya kuondokana na hali hiyo ili hatimaye kuhakikisha kuwa wafanyabiashara wa Tanzania hawakumbani na changamoto au uchelewaji wa kupata huduma hapa nchini.” alisema Nyaisa.
Nyaisa alitolea mfano kuwa BRELA imekuwa ikikutana na changamoto katika utendaji na kusababisha usumbufu kwa wateja, pale ambapo Taasisi za Udhibiti zimekuwa zikitoa vibali vya biashara bila kujiridhisha endapo mfanyabiashara huyo amesajili kampuni au jina la biashara.
Alisema kuwa athari kubwa anayoweza kuipata mfanyabiashara huyo endapo atapatiwa kibali wakati hajasajili Kampuni au Jina la Biashara ni kushindwa kusajili jina la biashara au kampuni endapo jina husika litakuwa na ufanano na majina yaliyokwisha sajiliwa BRELA, hivyo mhusika kulazimika kubadilisha jina husika.
Nyaisa alisema kuwa athari kubwa anayoipata mfanyabiashara anaposhindwa kusajili jina linaloonekana kwenye Kibali alichokipata, huathiri biashara yake kama vile kukosa zabuni, mikopo au kuingia mikataba na Taasisi za Umma.
Alisema kwa kuwa usajili wa jina la biashara au kampuni ni hitaji la msingi katika mfumo mpya wa ununuzi unaosimamiwa na Mamlaka ya Kudhibiti Ununuzi wa Umma (PPRA) uitwao Mfumo mpya wa kielektroniki wa manunuzi ya Umma (NeST).
Mfumo huo ambao umeunganishwa na mfumo wa usajili kwa njia ya mtandao ( ORS) wa BRELA, hivyo mfanyabiashara hataweza kujisajili katika mfumo wa NEST kama hajasajili Kampuni au Jina la Biashara.
Naye, Mkurugenzi wa Udhibiti Ubora kutoka Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Lazaro Msasalaga, alisema kuwa kikao kazi hicho ni muhimu maana kinatekeleza malengo ya BluePrint kwa kuzingatia umuhimu wa wafanyabiashara kuwa na Leseni ya Biashara inayotolewa na BRELA na leseni zingine zinazotolewa na Taasisi za Udhibiti ikizingatiwa kuwa sheria hizo zilikuwepo kabla ya andiko hilo.
BRELA, ilianzishwa chini ya Sheria ya Wakala za Serikali Na. 30 ya mwaka 1997 na kuzinduliwa rasmi Desemba 3, 1999 ikiwa chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara.
Majukumu ya BRELA ni pamoja na Kusajili majina ya Biashara, Kampuni, Alama za Biashara na Huduma, Utoaji wa Hataza, Utoaji wa Leseni za Biashara Kundi “A” na Utoaji wa Leseni za Viwanda na Vyeti vya Usajili wa Viwanda.