Brela yawarahisishia mambo wafanyabiashara

WAKALA wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela), wamejikita zaidi katika mitandao ya kijamii, ili kutanua wigo wa elimu ya usajili wa biashara na upatikanaji wa leseni kwa wafanyabishara na wawekezaji.

Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano Brela, Roida Andusamile, amebainisha hayo wakati akizungumuza na waandishi wa habari katika viwanja vya Bombambili mjini Geita, yalipo maonesho ya tano ya teknolojia ya madini.

Ametaja baadhi ya mitandao ya kijamii wanayoitumia kuwafikia watanzania ni facebook, twitter na

instagram ambayo imeongeza nguvu ya upatikanaji wa taarifa, ambazo awali zilipatikana kupitia vituo vya runinga, redio na magazeti.

“Kwa hiyo tunajitahidi sana kutumia mitandao ya kijamii kuhakikisha kwamba wadau mbalimbali wanatufikia na wanapata taarifa za Brela kupitia njia mbalimbali na sasa hata kwenye makundi ya WhatsApp tunafika.

“Hivyo hatuko nyuma kwenye suala la mitandao ya kijamii, tunaitumia ipasavyo kuhakikisha wananchi wanaelewa huduma tunazotoa kama wakala wa usajili wa biashara na leseni na ikizingatiwa kwamba usajili wetu ni kwa njia ya mtandao,” amesema na kuongeza:

“Tunawasihi Watanzania warasimishe biashara zao, na urasimishaji wa biashara ni kwa njia ya mtandao, kwani Brela tunatoa usajili kwa njia ya mtandao kwa hiyo mtu anachotakiuwa kufanya ni kuingia kwenye wovuti ya Brela.

“Unaposajili biashara, unaposajili kampuni, ile kuaminika kunaongezeka, na fursa mbalimbali unaweza ukapata kupitia usajili wa majina ya biashara, au kusajili kampuni, kwani mtu anakuamini kwamba anaweza hata akakukopesha.”

Mkuu wa Wilaya ya Nyang’hwale mkoani Geita, Jamuhuri William, amewaomba Brela kuendelea kutoa hamasa kwa wajasiriamali wadogo, ambao wengi wao bado wanafanya kazi na kuzalisha bidhaa pasipo kusajili nembo na chapa ya biashara.

 

Habari Zifananazo

Back to top button