WANANCHI wa Jimbo la Buchosa Wilaya Sengerema mkoani Mwanza wanatarajiwa kuanza kilimo cha zao la parachichi kutokana na mazingira ya eneo hilo kuwa na mvua nyingi na ardhi yenye rutuba.
Mbunge wa jimbo hilo, Eric Shigongo akiwa katika mkutano wa hadhara wa kusikiliza na kutatua kero za wananchi katika kijiji cha Iseng’he Kata ya Luharanyonga amewaeleza wananchi wa jimboni hapo kuwa zao hilo ni miongoni mwa mazao yenye faida kubwa.
Shigongo amesema kuwa wananchi wa Buchosa wamejikita kulima zao la miti ya mbao kama zao la biashara ambalo linachukuwa muda mrefu ili kufikia kiwango cha kuvuna lakini zao la parachichi ni kati ya miaka mitatu hadi minne tu na kuanza kuvuna.
Mazao mengine ya chakula na biashara yanayolimwa kwa wingi katika Jimbo la Buchosa ni mpunga ,mahindi, viazi na mihogo hivyo likiongezeka zao la parachichi litakuwa zao la kibihashara kutokana na muda wake mfupi kuanza kupata faida.
Aidha Shigongo aliongeza kuwa hali ya hewa ya Buchosa inafafana na hali iliyoko Mkoa wa Njombe unaolima zao la parachichi kwa wingi hivyo wamekubaliana na kamati ya fedha na mipango ya halmashauri ya Buchosa kuanza kilimo hicho cha zao la parachichi na wanatarajia kuanza kugawa mbegu siku sio nyingi ili wananchi wa jimbo hilo waweze kunufaika na kuondokana na umasikini kupitia zao hilo
“Tutaweka utaratibu madhubuti wa kupata miche hiyo ya parachichi kupitia halmashauri yetu na wananchi wataendelea kununua hapa kwa bei nafuu,”alisema Shigongo.