MWANZA: HOSPITALI ya Rufaa ya Kanda Bugando mkoani Mwanza imeiomba Serikali na wadau mbalimbali wa maendeleo kuiunga mkono katika mradi wa ujenzi wa jengo la mama na mtoto kwa lengo la kuokoa maisha ya watoto njiti.
Wito huo umetolewa leo, Ijumaa, na mkuu wa idara ya watoto katika hospitali hiyo, Neema Kayange wakati wa maadhimisho ya siku ya kimataifa ya watoto njiti duniani yaliyofanyika katika viwanja vya hospitali hiyo.
‘’Tunaomba sana serikali, wadau mbalimbali na uongozi wa hospitali ya Bugando itusaidie katika ujenzi wa jengo la wodi ya mama na mtoto,’’ amesema.
Amesema kwa mwezi mmoja hospitali ya Bugando inapokea watoto 130 kutoka mkoa wa Mwanza ambao wanazaliwa kwa wiki tofauti.
‘’Watoto wengi tunaohudumia wengi hawajafikisha wiki 37 za kukaa katika tumbo la mama na watoto wengi wanazaliwa kuanzia wiki 28. Bado tuna changamoto kubwa nafasi iliyopo katika hospitali yetu ni ya kuhudumia watoto 40,’’ amesema.
Akielezea chanzo chanzo kikubwa cha akina mama wengi kujifunga kabla ya wakati ni mambukizi ya bakteria, malaria, maambukizi ya njia ya mkojo (U.T.I) pamoja na mama mjamzito akiwa na mimba ya watoto mapacha.
Amesema upungufu wa damu kwa wa mama wajawazito haswa wakati wa ujauzito nayo huchangia tatizo hilo.
Kayange amewaomba wanawake wajawazito kuhudhuria kliniki kuanzia mimba inapokuwa changa kabisa na wajawazito wanatakiwa kupata lishe kamili.
Naye kaimu mkurugenzi wa hospital ya rufaa ya Bugando, Bahati Wajanga alisema eneo la kuhudumia watoto njiti katika hospitali yao ni dogo sana.
Ameahidi wapo katika maandalizi ya kujenga wodi mpya kwajili ya jengo la mama na mtoto na tayari hospitali yao ishatenga fedha.
Ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuboresha huduma za afya.
Naye mkazi wa mkoa wa Mwanza, Jamila Kaijage ameishukuru hospitali ya rufaa ya kanda Bugando kwa kuweza kumhudumia mtoto wake ambae kwa sasa ana kilo sita.
Comments are closed.