Bunge kuchagua wabunge A. Mashariki leo

BUNGE la Tanzania Alhamis  linatarajiwa kuchagua wabunge tisa wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA).

Katibu wa Bunge, Nenelwa Mwihambi alisema juzi kuwa wagombea 20 watashiriki uchaguzi huo wakiwa kwenye makundi manne likiwemo la wagombea wanawake, wagombea wa Zanzibar, wagombea wa vyama vya walio wachache bungeni na wagombea wa Tanzania Bara.

Mwihambi aliwataja wagombea hao kuwa ni Angela Kizigha (CCM), Nadra Juma Mohammed (CCM), Dk Shogo Mlozi (CCM), Queen Lugembe (CUF), Sonia Magogo (CUF) na Zainab Abdul (CUF) watagombea kupitia kundi la wanawake.

Watakaogombea kundi la Zanzibar ni Dk Abdulla Hasnuu Makame (CCM), Machano Ali Machano (CCM), Anderson Ndambo (CUF), Husna Mohamed Abdallah (CUF) na Mohamed Habib Mnyaa (CUF).

Aliwataja watakaogombea kupitia kundi la vyama vya walio wachache bungeni kuwa ni Ado Shaibu (ACT-Wazalendo), Jafar Saidi Mneke (CUF) na Mashaka Ngole (CUF).

Mwihambi aliwataja watakaogombea kupitia kundi la Tanzania Bara kuwa ni Ansar Kachwamba (CCM), James Millya (CCM), Dk Ng’waru Maghembe (CCM), Adui Kondo (CUF), Mohamed Ngulangwa (CUF) na Thomas Malima (CUF).

Uchaguzi wa wajumbe hao utafanyika leo bungeni ili kuchagua wajumbe tisa watakaokwenda kuwakilisha katika Bunge hilo la Afrika Mashariki na kati ya hao tisa nane ni kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) na mmoja kutoka vyama vingine.

Kuhusu kinachoendelea ndani ya Chama cha Wananchi (CUF) kuhusu majina ya wagombea wao, Katibu Mkuu alisema amesikia na ofisi yake ilifuatilia na kugundua taratibu zote zilifuatwa kuwakilisha majina ya wagombea hao na kuwa kinachoendelea sasa ndani ya CUF ni ndani ya chama chao.

 

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button