DODOMA: LEO Bunge litaanza kupokea na kusikiliza maoni ya wadau kuhusiana na Muswada wa Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani, Muswada wa Sheria ya Tume ya Uchaguzi na Muswada wa Sheria wa Vyama vya Siasa ya Mwaka 2023.
Miswada hiyo ilifikishwa bungeni na kusomwa kwa mara ya kwanza Novemba 10, mwaka jana na sasa bunge litakuwa na siku tatu za kusikiliza maoni ya wadau kuanzia leo, keshokutwa na Januari 10, mwaka huu.
Kwa mujibu wa taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria mkutano utaanza saa nne asubuhi katika ukumbi wa Frank Mfundo ghorofa ya tano katika jengo kuu la utawala, ofisi za bunge jijini Dodoma.
Hatua hiyo ya kupokea maoni inakuja kipindi ambacho Tanzania iko katika maandalizi ya kuelekea katika uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu na uchaguzi mkuu mwakani.
Baadhi ya wadau walisema kama sheria hiyo ikitumika vizuri inaweza kuwa sehemu ya upatikanaji wa Tume Huru ya Uchaguzi.
Muswada wa Sheria ya Tume ya Uchaguzi ya mwaka 2023 pamoja na mambo mengine, unatoa nafasi kwa wajumbe watano wa tume hiyo kuomba nafasi hiyo na mchujo utafanywa na kamati ya usaili tofauti na sasa wanateuliwa na rais bila kuomba.
Pia marekebisho hayo ya sheria yataondoa utaratibu wa wagombea wa ubunge kupita bila kupingwa na badala yake wagombea hao watapigiwa kura za ndio au hapana.
Aidha, muswada wa vyama vya siasa unampa msajili wa vyama vya siasa mamlaka ya kusimamia uchaguzi wa ndani wa vyama na michakato ya uteuzi wa wagombea wa nafasi mbalimbali za kisiasa kupitia vyama hivyo.
Pia unavitaka vyama vya siasa kutunza orodha ya wanachama wake ambayo muda wowote msajili wa vyama vya siasa anaomba apatiwe na chama kikishindwa kufanya hivyo kinaweza kusababisha chama kisimamishwe kufanya shughuli zake.
Aidha, muswada unamtaka mtu au taasisi yoyote inayotaka ama kutoa mafunzo ya elimu ya uraia kwa mwanachama wa chama fulani au kuwajenga uwezo, itoe taarifa katika ofisi ya msajili ambaye anaweza kuruhusu ama kusitisha suala hilo na kutoa sababu za kufanya hivyo.
Muswada pia unampa mamlaka msajili ya kukifuta chama chochote anachodhani kilipata usajili wake isivyo sahihi.
Maoni ya miswada hiyo yanakusanywa ikiwa zimepita siku mbili baada ya wadau wa siasa na demokrasia kukutana katika mkutano maalumu wa baraza la vyama vya siasa kujadili miswada ya sheria hizo.
Katika mkutano huo maalumu, wadau mbalimbali wameonesha kuguswa na muswada huo na wengi wamepongeza kitendo cha kusikiliza maoni.
Wakili Alex Mgongolwa alisema ni sheria itakayokuja kupunguza mapungufu kwenye NEC (Tume ya Taifa ya Uchaguzi) na kubadilisha muundo na hata sifa za mkurugenzi wa uchaguzi.
Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi Tanzania (UWT), Mary Chatanda alisema wanataka usawa wa kijinsia kwamba mwenyekiti wa tume ya uchaguzi kama akiwa mwanaume basi msaidizi wake awe mwanamke.
Mwenyekiti wa Chama cha UDP, John Cheyo alisema katika sheria kusiwepo na matumizi ya fedha katika uchaguzi ili kuwe na usawa kwa watu wote.
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha NCCR Mageuzi, Joseph Selasini alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuruhusu wadau kutoa maoni yao juu ya Tume ya Uchaguzi.
“Wadau wajikite zaidi kwenye kutoa maoni yao badala ya kutoa kasoro,” alisema Selasini.
Kwa upande wake Mhadhiri Mwandamizi Chuo Kikuu Mzumbe, Dk Mrisho Mbegu alisema ni muswada unaobainisha dhana nzima ya kuongozwa kwa ushirikishwaji katika kupata wajumbe.
Alisema ni muswada muhimu katika kupata viongozi bora, na pia kupunguza mamlaka na madaraka ya Rais katika uteuzi wa wajumbe.
Naye Dk Hilda Lyatonga alisema sheria ya NEC itasaidia kutoa tume huru iliyokuwa inahitajika na Watanzania wengi.