Bunge kuridhia azimio kuzuia ugaidi Afrika

MKUTANO wa nane wa Bunge unaendelea ambao pamoja na shughuli nyingine, leo litawasilishwa Azimio la Bunge kuridhia itifaki ya Mkataba wa Umoja wa Afrika wa kuzuia na kupambana na ugaidi ya mwaka 2004.

Ratiba inaonesha kesho pia itawasilishwa Azimio la Bunge la kuridhia itifaki  ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya kuongeza Mamlaka ya Mahakama ya Afrika Mashariki  wakati Septemba 21 Bunge litapokea taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo.

Aidha, Septemba 22 wabunge watamuuliza maswali Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na baadaye siku hiyo utafanyika uchaguzi wa wabunge wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA) na Septemba 23 baada ya maswali mkutano huo utahitimishwa kwa hoja ya kuuahirisha.

Katika mkutano huu wa bunge wa wiki mbili, tayari miswada mitatu imepitishwa bungeni jijini Dodoma ambayo ni Muswada wa Sheria ya Usimamizi wa Maafa wa mwaka 2022, Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali na wa Marekebisho ya Sheria ya Usimamizi wa Rasilimali za Maji wa mwaka 2022.

Septemba 16 mwaka huu, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba alipangiwa kuwasilisha Azimio la Bunge kuridhia kufuta hasara/upotevu wa fedha na vifaa vya serikali kwa kipindi  kinachoishia Juni 30, mwaka huu lakini muda ulipofika, Naibu Spika Mussa Azan Zungu aliahirisha bunge hilo mpaka leo.

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button