Bunge laagiza magati zaidi ya kisasa Bandari Dar

BUNGE limeielekeza Serikali kiharakishe utaratibu wa kuongeza magati ya kisasa na ufanisi wa Bandari ya  Dar es Salaam kabla ya ujenzi wa Reli ya Kisasa haujakamilika.

Haya yamebainishwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mitaji ya Umma(PIC), Jerry Silaa wakati wa kuwasilisha maazimio hayo.

Silaa alisema pia serikali iharakishe utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo.

Advertisement

Alisema changamoto ya SGR kutokupata mzigo wa kutosha kusafirishwa ni jambo litakalokwamisha kupatikana kwa tija ya uwekezaji uliofanyika.

Pia Bunge limeazimia kwamba, Serikali ihakikishe kuwa mazungumzo yanayoendelea katika Kamati ya Majadiliano ya Serikali (GNT) yafikie mwisho ndani ya miezi mitatu au yapelekwe Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC).

Kuhusu upungufu wa mtaji wa Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL), Bunge limeazimia kwamba Wakala ya Ndege za Serikali Tanzania (TGFA) kukamilisha agizo la Rais Samia Suluhu Hassan la kurudisha ndege kwa ATCL kwani Shirika Hilo linauwezo wa kujiendesha kwa faida.

Pia Bunge limeazimia kwamba, Serikali itekeleze ahadi yake  waliyoitoa kwa Benki ya Maendeleo ya Kilimo ya (TADB) ya kuiongezea mtaji kiasi Sh billion 100 kwa kila mwaka wa fedha, lengo likiwa ni kuongeza ufanisi na tija katika Sekta ya Kilimo.

Bunge limeazimia kwamba, serikali iharakishe utekelezaji wa ahadi yake ya kulipa deni Sh bilioni 21.8  la Pamba.

“Hatua hiyo itasaidia kuongeza ufanisi wa sekta hiyo na kurudisha taswira chanya ya Bodi ya Pamba.”

Alisema Bunge limeazimia kwamba, serikali itekeleze haraka agizo la kurejesha jukumu la Ujenzi wa Viwanja vya ndege kwa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege – TAA na Rasilimali zake zote ikiwamo watumishi waliohama mwaka 2017.

Alisema Bunge limeazimia serikali ikamilishe mchakato wa Public Key Infrastructure (PKI) na iunde mfumo wa taarifa wa pamoja kuondoa udanganyifu wa mifumo ya taasisi.

Pia Serikali ihakikishe inasimamia kikamilifu taasisi na mashirika ya umma kuimarisha mifumo ya TEHAMA,

Hatua hizi itasaidia kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma, ukusanyaji wa mapato, kupunguza matumizi yasiyo ya lazima na kudhibiti udanganyifu kwa lengo la kupata tija iliyokusudiwa.

Alisema Bunge limeazimia kwamba, Serikali ihakikishe mali zote za Kampuni ya Meli (MSC) zilizopo TPA zinarejeshwe haraka sana MSC zikiwemo cherezo, karakana na zinginezo.

Bunge linaazimia kwamba, Serikali ihakikishe Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) inaandaa mfumo madhubuti wa TEHAMA na kuanza kuutumia haraka iwezekanavyo kwa lengo la kuboresha utoaji wa huduma wa mfuko na kuziba mianya ya udanganyifu.

Alisema Bunge linaazimia kwamba, Serikali ielekeze ATCL na Shirika la Bima la Taifa (NIC) kufanya zabuni shindanishi ili kupata wakala mwenye bei nafuu, huduma bora na ambae atazingatia uwiano wa ndege shirika inazomiliki.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *