Bunge laagiza uchunguzi mkataba wa matrekta

SPIKA wa Bunge, Dk Tulia Ackson ameagiza ufanywe uchunguzi kuhusu changamoto na athari za mkataba wa mauziano ya matrekta ya Kampuni ya USAS kati ya Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) na wakulima nchini.

Akisoma taarifa bungeni Dodoma jana, Dk Tulia ameagiza Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji, Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo kukutana na wizara za Kilimo, Uwekezaji, Viwanda na Biashara na NDC kujadili changamoto na athari za mkataba huo kwa wakulima.

Ameelekeza kamati hiyo ikutane na wizara hizo kujadili changamoto na athari zilizowapata wananchi wakati wa utekelezaji wa mkataba wa ununuzi wa matrekta ya USAS na NDC ulifanyika kwa njia ya mauziano.

“Naelekeza kamati ikutane na Wizara ya Viwanda, Biashara na Kilimo na NDC na baada ya hapo, kamati itasafiri kwenda Manyara ili kusikiliza wananchi walioathirika na mikopo hiyo na kupata taarifa ya kina kuhusu changamoto na athari za mkataba huo,” alisema.

Dk Tulia alisema utaratibu wa mkataba wa mikopo ya matrekta ya USAS na NDC iliibua mijadala wakati wa kujadili Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu mwaka 2023/2024 na wabunge kwa niaba ya wananchi walilalamikia mkataba wa USAS na NDC na wakulima walipata changamoto na athari katika utekelezaji wake.

Amemuagiza Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Kilimo na Mifugo, David Kihenzile abaini tatizo la jambo hilo.

Dk Tulia alisema inawezekana suala hili linagusa mikoa mingine, lakini kutokana na changamoto ya bajeti, ametaka kamati iende Manyara kama mkoa wakilishi.

Ili Bunge lipate mrejesho kamili, baada ya kukamilisha uchunguzi huo, ameagiza kamati iandae taarifa na kuiwasilisha bungeni wakati wa siku sita za mwisho za Bunge la Bajeti kwa mujibu wa Kanuni ya 142.

Alisema wabunge watalipa Bunge suluhisho na hivyo wataishauri serikali kuhusu changamoto ya matrekta hayo na namna ulivyoibua changamoto kwa wakulima.

Dk Tulia alisema wabunge kwa niaba ya wananchi na mikataba hiyo wanaruhusiwa kwenda kamati ilipo wakatoe changamoto na athari za mikataba zilizojitokeza.

Habari Zifananazo

Back to top button