Bunge laelezwa fursa vivuko Kigamboni

DODOMA: BUNGE limeelezwa kuwa kuna fursa katika uendeshaji wa vivuko katika eneo la Kigamboni – Kivukoni mkoani Dar es Salaam.

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amesema bungeni Dodoma wakati akiwasilisha mpango na makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2024/25. Bashungwa alisema kwa sasa Kigamboni ina wakazi zaidi ya 300,000 na wanaotumia usafiri wa vivuko ni wastani wa watu 60,000 kwa siku.

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa

Amesema ili kuhudumia idadi hiyo ya watumiaji kwa vivuko, Wakala ya Ufundi na Umeme (Temesa) inashirikiana na kampuni ya Azam Marine Company Ltd kwenye utoaji wa huduma kivukoni hapo.

SOMA: Bashungwa awaondoa hofu watumia vivuko Dar

Aidha, Bashungwa amesema wizara inaendelea kuangalia utaratibu mzuri wa ushirikiano huo ili kutoa huduma kwa ufanisi zaidi na tija kwa pande zote mbili.

“Wizara inaendelea kuangalia utaratibu mzuri wa ushirikiano huo ili kutoa huduma kwa ufanisi zaidi na tija kwa pande zote mbili,” amesema.

Ameongeza, “matarajio ya Wizara ni kuwa ifikapo Agosti, 2024 Azam Marine watatoa huduma masaa 24 kwa siku sambamba na Temesa”.

Ametoa wito kwa wawekezaji wengine wenye nia kushirikiana na Temesa katika utoaji wa huduma za vivuko katika maeneo mengine nchini. Bashungwa alikaribisha wawekezaji waingie ubia na Temesa katika matengenezo ya magari na ukodishaji wa mitambo.

Mei 28, 2024 alipofanya mahojiano na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) Waziri Bashungwa alisema kuwa serikali imejipanga kuhakikisha inaimarisha huduma ya usafiri wa vivuko nchini.

“Niwatoe wasiwasi Wananchi wa Dar es salaam pamoja na Kigamboni, taharuki ambayo imetengenezwa hakukuwa na sababu ya kutengenezwa. Lakini sisi tunao fahamu yapo maslahi binafsi nyuma ya utengenezaji wa hii taharuki,” amesema Bashungwa.

Ameeleza kuwa, sasa vivuko vingi vinaendelea na matengenezo, lakini pia Mkandarasi Songoro Marine anaendelea na ujenzi wa vivuko vipya katika karakana yake mkoani Mwanza kwaajili ya kupelekwa kwenye maeneo mbalimbali kutoa huduma kwa wananchi.

Katika hatua nyingine, mnamo Novemba 11, 2022 Rais Samia Suluhu Hassan akiwa Kigamboni, alithibitisha kuwa Mkoa wa Dar es Salaam mesema itaingia mkataba na sekta binafsi kwa ajili ya uendeshaji wa kivuko cha Kigamboni lengo ikiwa ni kuongeza ufanisi na kurahisisha upatikanaji wa huduma hiyo kwa wananchi,

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa mradi wa maji Kigamboni, Rais Samia amesema kwa sasa kuna kivuko kidogo cha mtu binafsi kinachosaidia kutoa huduma kati ya Dar es Salaam na Kigamboni baada ya vivuko vikubwa kupata hitirafu.

Habari Zifananazo

Back to top button