Bunge laelezwa misingi sita uhusiano kimataifa

WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Stergomena Tax ametaja misingi sita ya Tanzania katika uhusiano kimataifa.

Dk Tax ameitaja misingi hiyo bungeni Dodoma jana wakati anawasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2023/24.

Alisema Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kuzingatia misingi iliyowekwa na waasisi wa taifa kusimamia uhusiano wa kimataifa

Dk Tax alisema misingi hiyo inapinga na kulaani vitendo vya uonevu na ukandamizaji popote duniani na kulinda uhuru wa kujiamulia mambo wenyewe.

Alitaja misingi mingine ni kulinda mipaka ya nchi, kutetea haki, kuimarisha ujirani mwema na kutekeleza sera ya kutofungamana na upande wowote.

“Misingi hii ndio dira na msimamo wetu kwenye uhusiano na nchi nyingine katika Jumuiya za kikanda na kimataifa,” alisema Dk Tax.

Aliongeza: “Misingi hii imeifanya nchi yetu kuendelea kupaza sauti katika majukwaa ya kimataifa, kushawishi mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi ulimwenguni, na kuweka mazingira yanayowezesha ustawi wa nchi zinazoendelea.”

Dk Tax alisema azma ya Tanzania ni kuwa na dunia yenye usawa, haki na amani ili kuchangia kuwepo kwa ukuaji wa uchumi shirikishi na maendeleo endelevu katika mataifa yanayoendelea, na yaliyoendelea kwa ustawi wa wananchi.

“Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaendelea kuunga mkono jitihada za kikanda na kimataifa katika kutatua na kutafuta suluhu ya changamoto zinazoikabili dunia ikiwemo umasikini, magonjwa ya mlipuko, mabadiliko ya tabianchi, migogoro, ugaidi na uhalifu unaovuka mipaka,” alisema.

Kuhusu siasa, ulinzi na usalama wa dunia, Dk Tax alisema kuwa baadhi ya nchi zimeendelea kukabiliwa na migogoro inayosababishwa hasa na tofauti za kiitikadi, kudorora kwa uchumi, ugaidi na machafuko ya kisiasa.

“Hali ya ukosefu wa amani, usalama na umaskini wa kipato vimeendelea kuwa chanzo cha maelfu ya watu kuyakimbia mataifa yao, na hivyo kusababisha ongezeko la wakimbizi na wahamiaji haramu.

Hali hiyo imesababisha ongezeko la uhalifu unaovuka mipaka, hususani biashara haramu ya usafirishaji wa binadamu,” alisema Dk Tax.

Habari Zifananazo

Back to top button