Bunge limeurejesha Muswada wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote ya mwaka 2022 kwa Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kwa mashauriano zaidi.
Awali ratiba ilionesha kuwa leo, Ijumaa, wabunge walitakiwa kujadili na kuupitisha muswada huo kabla ya Rais kuusaini na kuwa Sheria kamili.
Kabla ya kuanza kwa kipindi cha Maswali na Majibu bungeni leo asubuhi, Spika Dk Tulia Ackson amewatangazia wabunge kuwa muswada huo hatua hiyo imefikiwa kutokana na hoja za wabunge na wadau waliofika mbele ya Kamati kutoa juu ya suala hilo.
“Muswada utapelekwa Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii. Muswada huu utaletwa tena baadaye baada ya mashaurino,” amesema Spika.
Kwa mujibu wa waraka wa Wizara ya Afya juu ufafanuzi wa Muswada huo, Kupitia Sheria inayopendekezwa, Waziri mwenye dhamana ya masuala ya afya kupitia Kanuni ataweka viwango vya uchangiaji kwa kuzingatia uhitaji wa huduma, gharama halisi za matibabu na uwezo wa wananchi kuchangia na mapendekezo yaliyopo yatategemea maoni ya wananchi na ridhaa ya mamlaka zingine.
“Kupitia Sheria inayopendekezwa, watu wasio na uwezo watakuwa na haki ya kupata huduma za matibabu kupitia utaratibu uliowekwa na Serikali baada ya kuwatambua kupitia mfumo wa utambuzi wa watu wasio na uwezo wa Serikali,” ufafanuzi huo umeeleza.