BUNGE leo limeridhia Itifaki ya Biashara ya Huduma ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ya mwaka, 2012.
Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Ashatu Kijaji aliwasilisha leo bungeni maelezo kuhusu Azimio la Kuridhia Itifaki ya Biashara ya Huduma ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika ya mwaka, 2012 (SADC Protocol on Trade in Services, 2012).
Akiwasilisha maelezo hayo amesema wakuu wa nchi na Serikali wa SADC walisaini Itifaki ya Biashara ya Huduma tarehe 18 Agosti, 2012 Maputo, Msumbiji.
“Baada ya Itifaki ya Biashara ya Huduma kusainiwa, nchi wanachama zilianza awamu ya kwanza ya majadiliano ya ulegezaji wa masharti ya biashara ya huduma na kukamilisha awamu hiyo mwezi Juni 2019.
“Majadiliano hayo yalihusisha sekta 6 za kipaumbele ambazo ni mwasiliano, fedha, utalii, uchukuzi, nishati na ujenzi. sekta hizo zilichaguliwa kwa kuzingatia mchango wake katika maendeleo ya uchumi ya nchi wanachama na kiwango cha mtangamano baina ya nchi wanachama katika sekta hizo.
“Awamu ya pili ya majadiliano yaliyoanza Oktoba 2022 na bado yanaendelea yanahusisha sekta sita zilizosalia ambazo ni huduma za biashara; usambazaji; elimu; mazingira; afya ya jamii; burudani, utamaduni na michezo, “ amesema Waziri Kijaji.
Amesema nchi wanachama zilianza kuridhia Itifaki hiyo baada ya majadiliano ya awamu ya kwanza kukamilika Aprili, 2019 na hadi Januari 2022 jumla ya nchi wanachama 11 kati ya 16 sawa na theluthi mbili (2/3) ya Nchi wanachama wa SADC tayari zilikuwa zimeridhia Itifaki hiyo na hivyo kuipa nguvu ya kisheria kuanza kutekelezwa.
Amezitaja nchi ambazo hazijaridhia Itifaki hiyo ni Tanzania, Angola, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Madagascar na Comoro.
Comments are closed.