Bunge laridhia itifaki kudhibiti vitendo vya kigaidi

BUNGE limeridhia Itifaki ya Mkataba wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika wa Kuzuia na Kupambana na Ugaidi ya Mwaka 2004 ili kudhibiti vitendo vya kigaidi.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni aliwasilisha azimio hilo bungeni jijini hapa jana.

Masauni alisema kuna vikundi vimekuwa vikieneza itikadi za msimamo mkali za kuwashawishi watu kujiunga na makundi ya kigaidi na kuwa dalili hizo zinaifanya nchi kuwa katika hatari ya kuathiriwa na harakati za vikundi hivyo.

Alitoa mfano wa tukio la kigaidi lililotokea Uganda mwaka 2010 na kuwa watuhumiwa wawili ambao ni raia wa Uganda walikamatwa Tanzania na kurudishwa huko.

Masauni alisema pia kumekuwa na matukio yenye viashiria vya ugaidi ndani ya nchi ambavyo vimejitokeza katika mikoa ya Arusha, Geita, Mwanza, Pwani na Tanga.

Aliwaeleza wabunge kuwa pia kuna za kuenea kwa itikadi za msimamo mkali zinazosababisha watu kuhamasika na kujiunga na vikundi vya kigaidi na vikundi vyenye misimamo mikali nje ya nchi hivyo ni muhimu Tanzania iridhie itifaki hiyo.

Alisema Tanzania imechukua hatua kupambana na ugaidi kama vile kutungwa kwa Sheria ya Kuzuia Ugaidi ya Mwaka 2002, kushirikiana na nchi jirani kulinda mipaka.

Pia kuanzisha Kituo cha Taifa cha Kuratibu Mapambano Dhidi ya Ugaidi kinachoundwa na maofisa wa vyombo vya ulinzi na usalama, na kuwa na mfumo mahsusi wa kutafuta, kuchakata na kubadilishana taarifa za kiintelijensia

Alisema mwaka 2004 ilianzishwa Itifaki ya Mkataba wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika wa Kuzuia na Kupambana ikiwa ni katika kuzingatia Ibara ya 21 Ibara Ndogo ya Kwanza ya Mkataba wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika wa Kuzuia na Kupambana na Ugaidi wa mwaka 1999 na Tanzania ilisaini Itifaki hiyo Januari 27, 2005.

Alisema itifaki hiyo itaimairisha ulinzi na usalama wa raia na mali zao, nakurahisisha ubadilishanaji wa taarifa za kiintelijinsia zinazohusu ugaidi kupitia ushirikiano na nchi wanachama.

Nyingine ni kuongeza ujuzi kwa wataalamu nchini kupitia ubadilishanaji wa uzoefu na mafunzo na kuimarika kwa ushirikiano katika masuala ya urejeshwaji wa watuhumiwa wa ugaidi.

Aliyataja manufaa mengine kuwa ni kuwezesha nchi kushirikiana na nchi wanachama kulinda amani na usalama na kuhakikisha inalinda maisha ya watu na mali, kuwezesha kubadilishana wahalifu wa kigaidi kupitia makubaliano au mikataba maalumu.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama iliunga mkono itifaki hiyo.

Mwenyekiti wa kamati, Vita Kawawa alitaja faida ambazo Tanzania itazipata kwa kuridhia itifaki hiyo ni kuimarika shughuli za kiuchumi na kijamii kutokana na kuwepo kwa amani na usalama nchini, na kushirikiana na wanachama wengine kulinda amani na usalama.

Vita alitaja manufaa mengine kuwa ni kutumia njia za usuluhushi endapo kutatokea mgogoro kuhusu tafsiri na utekelezaji wa itifaki, kutumia itifaki hiyo kama mwongozo wa kisheria katika kuanzisha makubaliano na nchi wanachama ambazo hazina utaratibu wa kubadilishana wahalifu wa kigaidi.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Pindi Chana alisema kuridhiwa kwa itifaki hiyo kutauhakikishia umma na wageni kuwa Tanzania ni salama hasa katika masuala ya utalii.

Dk Chana alisema utalii umekuwa ukichangia asilimia 17 ya Pato la Taifa, ajira milioni 1.5 na fedha za kigeni kwa asilimia 25, hivyo amani na usalama ni muhimu.

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button