Bunge laridhia Itifaki ya Mahakama ya EAC

BUNGE limeridhia Itifaki ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ya kuongeza Mamlaka ya Mahakama ya jumuiya hiyo kwa lengo la kutekeleza majukumu ya kutatua migogoro ya kibiashara na uwekezaji.

Akiwasilisha Azimio la Kuridhia Itifaki hiyo bungeni Dodoma Jumanne, Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro aliomba Bunge kuridhia itifaki hiyo kutokana na kwamba serikali kupitia Baraza la Mawaziri lilipitisha mapendekezo ya kuridhia Agosti 31, mwaka huu.

“Lengo la kuridhia itifaki hiyo ni pamoja na kuongeza mamlaka ya Mahakama ya EAC ili iweze kutekeleza majukumu ya kutatua migogoro ya bidhaa na uwekezaji itokanayo na utekelezaji wa Itifaki ya Umoja wa Forodha, Itifaki ya Soko la Pamoja na Itifaki ya Umoja wa Fedha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki,” alisema Dk Ndumbaro.

Alisema matokeo ya kuridhiwa kwa itifaki hiyo ni kuwapatia fursa wananchi wanachama wa jumuiya kutumia Mahakama ya EAC katika kutatua migogoro itokanayo na mtangamano huo.

Dk Dumbaro alisema kutatua migogoro hususani wakati huu ambao nchi wanachama zimeridhia itifaki za uanzishwaji wa Umoja wa Forodha mwaka 2004, Soko la Pamoja (2010) na Umoja wa Sarafu (2013).

Kwa utaratibu wa sasa, endapo kunajitokeza mgogoro katika kutekeleza itifaki hizo, shauri lake hutakiwa kuamuliwa na mahakama ya nchi mwanachama ambako mgogoro umetokea, jambo linaloweza kusababisha kuwepo kwa tafsiri tofauti za itifaki hizo miongoni mwa nchi wanachama.

Ili kuondoa dosari za namna hiyo, ipo haja kuipa Mahakama ya Jumuiya ya Afrika Mashariki mamlaka ya kushughulikia mashauri yanayotokana na utekelezaji wa itifaki hizo ili kutoa tafsiri za kisheria zitakazotumika katika nchi zote wanachama wa jumuiya inapotokea utata hususani tafsiri ya vipengele mbalimbali vya itifaki hizo.

Dk Ndumbaro alisema hatua hiyo ya kuridhia itifaki ni muhimu hasa kunapotokea migogoro inayohusisha raia wa nchi zaidi ya moja wanachama au mali zisizohamishika zilizo nje ya nchi kulipotokea migororo.

Aidha, kuridhiwa kwa itifaki hii kutasaidia nchi wanachama kuepuka uwezekano wa migongano ya kisheria kutokana na tafsiri tofauti kwa kipengele kimoja.

Vilevile, kutoongeza fursa za ajira kwa Watanzania wa kada mbalimbali wakiwamo majaji.

Hadi kufikia Agosti 31, mwaka huu nchi wanachama nne zimeridhia itifaki ambazo ni Kenya, Uganda, Rwanda na Sudan Kusini. Tatu zilikuwa bado.

 

 

Habari Zifananazo

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x