Bunge ‘lasimama’ mjadala wa mahindi

SPIKA wa Bunge, Dk Tulia Ackson ametuliza mjadala wa wabunge waliokuwa wakilalamika kuwa Wakala ya Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) haina uwezo wa kununua mahindi ya wakulima. Wabunge walitaka serikali iruhusu wafanyabiashara kuuza popote wanapotaka bila kufuata utaratibu na kama inataka vibali vya kuuza popote vianze kutolewa mwakani.

Awali, kabla Dk Tulia kufafanua zaidi, Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe alisema serikali haijafunga mipaka. Alisema pia imeipa NFRA Sh bilioni 320 hivyo inachotaka ni kuhakikisha wafanyabiashara wanasajili kampuni zao na kuwa na vibali vya kusafirisha zao hilo popote.

Akihitimisha mjadala huo baada ya Bunge kusimamisha shughuli zake na kujadili hoja hiyo iliyotolewa na Mbunge wa Mombo, Condester Sichalwe (CCM). Mbunge huyo aliomba Bunge liazimie kwamba serikali ianze utaratibu wa kotoa vibali mwakani.

Dk Tulia alisema Waziri wa Kilimo, Bashe aliwaambia wabunge kuwa wanatakiwa kukumbuka changamoto walizozipitia mara kadhaa na wakati wote serikali ilichukua hatua na kupokea ushauri kwa ajili ya kusaidia wakulima.

“Niwakumbushe mambo machache, mwaka 2021 Bunge lilijadili hoja na ikatoa Sh bilioni 50 kwenda kununua mahindi ya wakulima. Hivi jambo hili lina sura mbili, serikali inapoweka utaratibu ni jambo jema na hata pale tukiishauri huwa inafanya kama ambayo ilitoa Sh bilioni 50 inatoa kununua mahindi sababu wananchi walibaki nayo hawakujua la kufanya nayo,” alisema.

Dk Tulia alishauri mahindi ambayo NFRA ilipewa Sh bilioni 320 ni kwa ajili ya kwenda kununua mahindi kipindi hiki wanayoweza kununua. Alishauri taarifa za vituo vilivyofunguliwa na wakala kwa ajili ya kununua mahindi vipewe msukumo wa kuanza kufanya kazi.

Aliwakumbusha wabunge faida ya kuhifadhi chakula NFRA kwamba mwaka jana baadhi ya wabunge walipata changamoto ya chakula katika majimbo yao. “Sisi tuwe na pande zote mbili si upande mmoja, lazima serikali iwe na chakula mahali ili ipeleke chakula katika maeneo yenye changamoto hivyo lazima inunue mahindi ili kuweka akiba,” alisema.

Awali Mbunge wa Momba, Condesta akihitimisha hoja yake baada ya wabunge kujadili na kutaka Bunge liazimie, aliomba serikali ianze utaratibu wa kutoa vibali vya usafirishaji mahindi mwakani.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba alisema serikali haijafunga mipaka isipokuwa wafanyabiashara wanatakiwa kufuata utaratibu wa kuwa na leseni ili kununua mazao na kupeleka wanakotaka.

Waziri wa Kilimo, Bashe pia alisisitiza kuwa serikali haijazuia wafanyabiashara kuuza mazao nje ya nchi. Alitoa mfano kuwa jana serikali iliruhusu tani 3,640 za mahindi kuuzwa nje na tangu Juni Mosi hadi 22, 2023, zaidi ya tani 32,000 zimeruhusiwa kuuzwa nje ya nchi kwa wafanyabiashara wenye vibali

Habari Zifananazo

1 Comment
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button