Bunge lataka busara taarifa za mauaji

SPIKA wa Bunge, Dk Tulia Ackson amelitaka Jeshi la Polisi litumie busara kutangaza taarifa kuhusu matukio ya mauaji.

Dk Tulia alitoa agizo hilo bungeni Dodoma Jumatano baada ya Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Khamis Hamza Khamis kujibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Cecilia Pareso (Chadema).

Pareso alitaka kufahamu mkakati wa serikali kudhibiti mauaji yaliyokithiri nchini.

Dk Tulia alisema haoni haja polisi kutoa taarifa kwa wananchi kuhusu mauaji kwa kuwa huenda zinachangia ongezeko la vitendo hivyo.

Alisema Jeshi la Polisi linafanya mambo mengi ya ulinzi nchini ambayo raia hawajui hivyo ni bora wasitoe taarifa kuhusu mauaji.

“Inatakiwa kuangalia namna nzuri ya kuwasiliana na wananchi badala ya kusambaza habari hizo na ndio matukio ya mauaji yamekuwa yakiongezeka,” alisema Dk Tulia.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Bunge na Uratibu), George Simbachawene alisema kuna umuhimu wa wadau wote kushiriki kutafuta na au kufanya utafiti sababu za mauaji.

Simbachawene alitaja baadhi ya sababu zinazotajwa kuchangia mauaji ni wivu wa mapenzi, imani za kishirikina, ugomvi wa ardhi na mipaka ya ardhi na kugombea mali na uhalifu mwingine.

Simbachawene alisema huenda maendeleo ya sayansi na teknolojia yanachangia kuonesha ukubwa wa tatizo hilo kwa kuwa upashanaji habari umeongezeka.

Awali Khamis alilieleza bunge kuwa kumekuwa na ongezeko la matukio ya mauaji nchini na mengi yanasababishwa na wananchi kujichukulia sheria mkononi, wivu wa mapenzi, migogoro ya ardhi, ulevi na imani za kishirikina.

 

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button