Bunge lataka mifumo kudhibiti ukatili kwa watoto

SPIKA wa Bunge, Dk Tulia Ackson ametoa rai kwa viongozi wa serikali kuimarisha mifumo ya kubaini vitendo au matukio ya ukatili na unyanyasaji dhidi ya watoto na hatua za kudhibiti vitendo hivyo.

Dk Tulia alitoa rai hiyo jijini Dodoma wakati wa utoaji zawadi kwa wanafunzi waliofanya vizuri kitaifa kwenye shindano la uandishi wa insha yenye ujumbe wa ‘Madhara ya mimba na ndoa za utotoni’.

Alisema serikali imeendelea kuchukua jitihada kuzuia mimba na ndoa za utotoni na kusisitiza kuwa Bunge lilitunga Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971 na marekebisho ya Mwaka 2009 na kuridhia mikataba ya kimataifa ya haki za mtoto.

“Bunge lipo tayari kupokea maoni mbalimbali ya wadau kuhusu haja ya kuboresha sheria hii ili kukidhi matakwa ya sasa.”alisema.

Pia aliwataka kuanzisha sanduku la maoni mashuleni ili wanafunzi, wazazi na wanajamii waaminifu walitumie kutoa taarifa za unyanyasaji na ukatili dhidi ya watoto na kuanzisha mabaraza ya watoto kama majukwaa ya kuwawezesha wanafunzi kujitambua na kuibua vitendo vya unyanyasaji na ukatili dhidi yao.

Aidha, Dk Tulia aliwataka kuzingatia maoni ya wanafunzi yanayopendekeza kuwa, viongozi wa dini wasikubali kufungisha ndoa za watoto wadogo na kuendelea kutoa elimu ya madhara ya mimba na ndoa za utotoni kupitia majukwaa mbalimbali.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Dk Festo Dugange alisema serikali kwa kushirikiana na wadau wa elimu nchini inaendelea kuchukua hatua stahiki kuhakikisha vitendo vya unyanyasaji na ukatili dhidi ya watoto ikiwemo mimba na ndoa za utotoni zinatokomezwa nchini.

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button