BUNGE la nchini Peru limemuondoa madarakani rais wa nchi hiyo, Pedro Castillo, kwa madai ya uhalifu, uasi na nia yake ya kutaka kuvunja bunge, huku nafasi yake ikizibwa na Dina Boluarte ambaye amekuwa rais wa kwanza mwanamke, baada ya kuapishwa jana jioni.
Bunge la Congress lilipiga kura za kutokuwa na imani na rais huyo, ambapo wajumbe 101 katika baraza la wabunge la watu 130 walipiga kura za ndio za kumshtaki kiongozi huyo.
Baada ya kupigwa kura hizo, Ripoti katika vyombo vya habari vya ndani zinasema alikuwa akielekea katika ubalozi wa Mexico katika mjimkuu na ndipo alipokamatwa na kushtakiwa kwa makosa ya uasi na uhalifu.
Castillo alijaribu kulivunja Bunge saa chache kabla ya kuanza kwa kesi mpya ya kumshtaki ikiwa ni kesi ya tatu tangu aingie ofisini Julai 2021.
Aidha, Boluarte, alikuwa makamu wa rais wa zamani wa nchi hiyo, aliapishwa nafasi hiyo ya juu katika Bunge la Congress na kuwa Rais wa sita wa Peru chini ya miaka mitano.
Kiongizi huyo ambaye pia ni wakili mwenye umri wa miaka 60, alisema atatawala hadi Julai 2026, wakati ambapo urais wa Castillo utakuwa umekamilika.
Akizungumza baada ya kula kiapo Boluarte alitoa wito wa kufikiwa kwa mapatano ya kisiasa ili kuondokana na mzozo ambao umeikumba nchi. “Ninachoomba ni nafasi, wakati wa kuokoa nchi,” alisema.
Katika hotuba yake kwa njia ya televisheni alisema: “Katika kukabiliana na matakwa ya wananchi katika marefu na mapana ya nchi, tumeamua kuanzisha serikali ya kipekee yenye lengo la kurejesha utawala wa sheria na demokrasia.
”
Alisema kuwa “Kongamano jipya lenye mamlaka ya kutunga katiba mpya” litaitishwa “katika muda usiozidi miezi tisa”.