Bunge: Wakandarasi miradi mikubwa waisaidie jamii (ya kimkakati)
KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imeishauri serikali ielekeze wakandarasi wanaotekeleza miradi mikubwa ya maendeleo waihudumie jamii ili wananchi wanufaike na uwepo wa miradi hiyo.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Selemani Kakoso alisema hayo wakati wa ziara kukagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa daraja la Wami mkoani Pwani.
Kakoso alisema ni muhimu miradi mikubwa iache alama kwa wananchi wanaoishi ya jirani na inapotekelezwa ili wananchi waone manufaa ya uwepo wa miradi hiyo.
Aliielekeza Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi iimarishe utunzaji wa mazingira ya eneo la daraja la Wami ili lidumu kwa muda mrefu.
Kakoso alisema ni muhimu mazingira ya eneo hilo yatunzwe ikiwamo miundombinu yake kwani serikali imewekeza fedha nyingi katika eneo.
“Niwaombe wananchi wa maeneo ya jirani na mradi nyie ndio muwe walinzi wa kwanza wa daraja kwa kutohujumu miundombinu ya daraja na kutoa taarifa za uwepo wa viashiria vya uharibifu ili hatua za haraka ziweze kuchukulia kwani mradi huu umelenga kuimarisha uchumi wanchi na maeneo ya jirani”alisema.
Ujenzi wa miradi hiyo ya madaraja ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020-2025 na Mpango wa Maendeleo
wa Taifa wa Miaka Mitano (2021/22 – 2025/26).
Naibu Waziri wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Godfrey Kasekenya alisema daraja jipya la Wami lina umuhimu katika uchumi wa nchi kwa kuwa litafungua fursa za kiuchumi kwa wananchi wa ukanda wa kaskazini na nchi kwa ujumla.
Kasekenya alisema serikali imekuwa ikiendelea kuboresha miundombinu ya barabara na madaraja ili kutoa fursa za kurahisisha shughuli za usafirishaji ikiwemo biashara kwa lengo la kuinua uchumi wa mwananchi mmoja mmoja nan chi kwa ujumla.
“Ujenzi wa daraja hili jipya ni katika kukamilisha changamoto ya daraja la awali ambalo lilikuwa halikidhi mahitaji ya magari yalikuwa yakipita kutoka na kuwa ni jembamba lakini hili la sasa linakwenda kumaliza changamoto hiyo ikiwemo kupunguza ajali”alisema Naibu waziri Kasekenye.
Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) Mkoa wa Pwani, Baraka Mwambage alisema daraja limekamilika kwa zaidi ya asilimia 97%.
Mwambage alisema mradi huo unatarajiwa kugharimu Sh bilioni 75.1 umeajiri wafanyakazi 420 wakiwamo Watanzania 395.
Ujenzi wa daraja jipya la Wami umetekelezwa kwa fedha za ndani na umesanifiwa lidumu kwa miaka 120.