SAFARI ya maisha ya beki wa kati wa timu ya soka ya Mtibwa Sugar, Iddy Mobby Mfaume, ilihitimishwa Machi 7, mwaka huu (2023) alipozikwa kwenye makaburi ya Mshikamano mkoani Shinyanga.
Mazishi yake yaliongozwa na Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB), Almas Kasongo pamoja na wadau mbalimbali wa mchezo wa mpira wa miguu kutoka mikoa jirani ya Mwanza, Kagera, Simiyu, Tabora na Mara.
Kocha Mkuu wa timu ya Mtibwa Sugar, Salum Mayanga anasema kuwa mchezaji huyo alikuwa tegemeo katika safu ya ulinzi na hiyo ilitokana na uwezo mkubwa aliokuwa nao na busara anapokuwa uwanjani.
Mayanga anasema tangu aanze kufundisha soka hajawahi kukutana na mchezaji mwenye busara na hekima kama Mobby na pia alikuwa ni msikivu.
Kocha huyo anamtaja Mobby kuwa ni mpenda ibada, kitu ambacho kilimfanya kuwa mfano kwa wachezaji wenzake.
“Sikuweza kumtumia mara nyingi tangu tumsajili mwanzoni mwa msimu huu kutokana na majeraha ya kifundo cha mguu aliyokuwa nayo, lakini nilimleta kwa kazi maalumu kutokana na uwezo na kipaji alichonacho. Mungu ampe kauli thabiti,” anasema Mayanga.
Naye Msemaji wa timu ya soka ya Mtibwa Sugar, Thobias Kifaru anasema klabu na uongozi wa Kampuni ya Sukari Mtibwa umempoteza mtu muhimu kwenye familia ya michezo nchini.
“Tumempoteza mchezaji mwandamizi, ambaye alitegemewa sana katika ukuaji wa soka nchini kutokana na mchango wake,” anasema Kifaru.
Nao wachezaji wenzake wa timu hiyo, Vitalis Mayanga pamoja na Mohamed Makaka kwa nyakati tofauti wanamuelezea marehemu kuwa mchezaji mpole anayeongea na kila mtu na hivyo kuishi vizuri na wenzake.
“Kwangu nilikuwa naye karibu na alikuwa ni ndugu yangu na rafiki wa wote na sisi wachezaji tutamkumbuka kwa mengi mema aliyoyatenda kipindi cha uhai wake,” anasema Makaka.
Mayanga yeye anasema kuwa Mobby atabaki moyoni kutokana na kuishi naye kwa upendo tangu walipojuana miaka kadhaa iliyopita wakiwa mkoani Shinyanga.
Anasema siku chache ambazo wamecheza pamoja katika timu ya Mtibwa Sugar amejifunza mambo mengi kutoka kwake, ikiwemo hekima na busara zake katika masuala mbalimbali.
“Mobby alikuwa ni mtu ambaye hapendi kumwona mwezake akifeli (kushindwa), ni mtu ambaye anapenda maendeleo na ni mpambanaji na alikuwa anahuruma sana, hivyo nikikumbuka inaniuma sana rohoni,” anasema Mayanga.
Nao wadau wa soka na wananchi wameendelea kumlilia mchezaji Mobby kutokana na kutambua mchango wake mkubwa kwenye familia ya mpira wa miguu nchini.
Kocha wa Rhino Rangers, Athuman Bilal anasema kuwa Tanzania imepata pigo kwa kumpoteza kijana mpambanaji na mpenda maendeleo katika soka.
Bilal anasema upambanaji wake ni kutokana na moyo wa kijasiri aliokuwa nao katika kulipigania Taifa na maisha yake ya soka.
“Inauma sana kiasi cha kutojua nianze wapi, lakini Mobby, ni kijana aliyekuwa na kiu ya maendeleo tangu namfundisha Toto Africans hadi Stand United, namjua vizuri sana,” anasema Bilal.
Mwalimu msaidizi wa timu ya Ruvu Shooting FC, Frank Msese kwa upande wake anasema wakati anaitumikia timu hiyo kwa nafasi yake, alifanikiwa kuiboresha timu na mchango wake uliisaidia sana timu hiyo.
Msese anasema timu ya Ruvu Shooting FC ilimsajili mchezaji huyo kwenye dirisha dogo la msimu wa mwaka 2021/2022.
Anasema walimtoa timu ya Geita Gold ya mkoani Geita kwenye dirisha dogo la usajili na baada ya kusajiliwa alikuwa ni msaada mkubwa kwa nafasi ya beki wa kati.
Msese anasema wakati anasajiliwa kuchezea timu hiyo ilikuwa kwenye nafasi ya 12 na kumaliza ligi ya msimu huo wa 2021/2022 kwa kushika nafasi ya 13.
“Kwenye nafasi yake aliweza kuiboresha timu na mchango wake kwa timu aliisaidia sana,” anasema Msese.
Anasema walimsajili mchezaji huyo kwa mkataba wa miezi sita kwa ajili ya kumalizia msimu wa ligi wa mwaka 2021/2022.
Msese anasema baada ya kumaliza msimu huo mkataba wake ulikuwa wazi kwa maana uliisha na yeye alipata timu nyingine ambayo ni Mtibwa Sugar.
“Kutoka hapo hadi mauti inamfika amekuwa kwenye timu ya Mtibwa Sugar …sisi Ruvu Shooting FC tutamkumbuka kwa mema, mazuri yake na mchango wake ambao alikuja kutusaidia kwenye timu yetu,” anasema Msese.
“Wakati tunamsajili tulikuwa na tatizo kidogo eneo la ulinzi, lakini alipofika yeye timu ikaimarika kutokana na uwezo wake wa uchezaji wa mpira, mchezaji ambaye sisi alitusaidia kwa kiasi kikubwa kutokana na ubora wake aliokuwa nao,” anasema Msese.
Msese anamtaja Mobby kuwa mchezaji mwenye uzoefu kutokana na kucheza ligi muda mrefu na pia kucheza kwake kwenye timu ya Taifa kwa nyakati tofauti.
“Ni mchezaji ambaye sisi Ruvu Shooting FC tunamkumbuka kwani alitusaidia sana na kifo chake kwa timu yetu kimetuhuzunisha kwa maana kimekuja ghafla na hatukutarajia kumpoteza mchezaji huyo katika kipindi hiki,” anasema.
Anasema mara nyingi mchezaji ambaye anafariki wakati bado anacheza mpira jambo hilo linasikitisha sana kwa sababu anakuwa malengo yake hajayafikia.
Msese amemtaja kuwa ni mpambanaji na sio mkataji wa tamaa, na hata kipindi cha uhai wake alikuwa kiongozi kwa wenzake.
Anasema Mobby alikuwa ni kiongozi kwa wachezaji wenzake na benchi la ufundi la timu lilikuwa linamtegemea kuhamasisha wenzake ili kuweza kufikia yale malengo.
“Lakini Mwenyezi Mungu amempenda zaidi na sisi tunasema tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa hilo lililotokea kwani ndiye mweza wa yote,” anasema Msese.
Anasema wanapaswa wajitambue kuwa mpira wa miguu ni kazi waliyoichagua, ni ajira na waifanye kwa umakini na weledi mkubwa wakizingatia maisha yao yapo kwenye mpira.
Naye Ally Kombo ambaye ni mchezaji kiungo mkabaji anasema, wamejawa na masikitiko makubwa ya kumpoteza aliyekuwa mchezaji mwenzao, licha ya kuhamia timu ya Mtibwa Sugar.
Kombo anasema wakati wote wakiwa na marehemu wakati wa uhai wake, walikuwa wakiishi kama ndugu.
“Ninakumbuka kwa kazi yake akiwa uwanjani alikuwa ni zaidi ya mchezaji, alikuwa ni mchezaji kiongozi, tunasikitika kwa kifo chake,” anasema Kombo.
Mobby alifikwa na umauti kwenye Hospitali ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma Machi 5, mwaka huu alipofikishwa kwa matibabu baada ya kujisikia vibaya akiwa katika mazoezi binafsi ya barabarani akijiandaa na mchezo wa Kombe la FA dhidi ya KMC.
Kwa mujibu wa daktari wa Hospitali ya Kampuni ya Mtibwa Sugar, Khalid Sabuni, Mobby alipata tatizo la kiafya Machi 4, 2023.
Mobby baada ya kufikwa na umauti mwili wake ulisafirishwa kwenda mkoani Shinyanga Mtaa wa Ndembezi, Kata ya Ndembezi Manispaa ya Shinganya na kuzikwa katika kaburi ya Mshikamano Machi 7, 2023.
Mazishi yake yalifanyika kwenye makaburi ya Mshikamano Machi 7, 2023 mkoani humo.
Mobby ameacha mke na mtoto mmoja na wakati wa uhai wake alizichezea timu mbalimbali za soka za Mwadui FC, Polisi Tanzania, Geita Gold, Ruvu Shooting FC zote za Ligi Kuu katika nyakati tofauti.
Pia alikuwa miongoni mwa mabeki wanaounda kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ na hadi mauti inamkuta alikuwa akiichezea timu ya Mtibwa Sugar.
Buriani Iddy Mobby Mfaume.