Buriani Peter Mwenda, umetuachia hazina

TUNAJUA kuwa siku yaja kwa kila mwanadamu, lakini hakujua itakuwa sasa, tulijua lazima siku itafika kwa kila mwanadamu, lakini bado kifo chake tumeshituka.

Ni Jumanne ya Agosti 15, 2023 saa 11 jioni simu yangu ya mkononi inaita, naangalia naona simu ya mtu ninayemheshimu sana, nikaipokea na haya yalikuwa sehemu ya mazungumzo yetu:

“Mgosi upo nyumbani kwako?” Alianza kwa kunihoji, nikamjibu hapana, ila kuanzia saa tatu usiku nitakuwa nimerudi.

Akanieleza kuwa afya yake si nzuri na anajua hizo taarifa sina, maana kama ningekuwa nazo ningefika kumuona, nikamuuliza tangu lini anaumwa? Akasema zaidi ya wiki sasa, ila kwa siku hiyo kidogo afya yake ilikuwa vizuri.

Nikamwambia sawa nitapita kumuona saa tatu usiku wakati narejea nyumbani.

“Kama ni saa tatu najua hiyo inaweza ikafika saa nne, nitakuwa nimepumzika, najua nawe utakuwa umechoka, siumwi sana usihofu, upitie asubuhi tutazungumza vizuri,” alinipa maelezo ambayo nilikubaliana nayo, kwani alinihakikishia afya yake ipo vizuri.

Jumatano saa 11:54 asubuhi, simu yangu ikaita na namba iliyopiga ni ile ile ya jana jioni, nikasema mawazoni mwangu kwa haraka zaidi kwamba pengine huyu Mzee anataka kunijulisha kuwa anaenda hospitali hivyo tuonane jioni.

“Hallow,” niliita na sauti ya upande wa pili ikapokea, lakini haikuwa sauti ya Mzee mwenye simu bali ya kijana wake aitwaye John.

“Kaka vipi salama? Aliuliza John, nikamjibu salama na kuongeza: “Nina ratiba ya kupita nyumbani hapo kuja kumcheki Mzee,” nilimwambia.

“Kaka Amir naomba nikujulishe Mzee Mwenda Inna Lillahi,” hata kabla hajamalizia nilimkatisha kwa kumuita jina lake John imekuwaje? Unazungumza kutoka wapi?

Alinieleza Mzee alizidiwa usiku, wakamkimbiza kliniki ya kisukari, kijana alitaka kunipigia simu usiku huo, lakini kwa namna alivyochanganyikiwa hata namba yangu hakuiona na hakujua aliisave vipi. “Sawa nimekuelewa John,”  nilimjibu na kukata simu.

Hivyo ndivyo nilivyopokea simu ya kifo cha mwanahabari nguli Peter Joseph Mwenda kilichotokea asubuhi ya Jumatano Agosti 16, 2023, ametutoka hatunaye kwa vile ametangulia kule ambako sote siku yetu ikifika tutamfuata.

Ameondoka duniani mchapa kazi mkubwa aliyeitendea haki tasnia ya habari za michezo, siasa, jamii na kila aina ya habari. Amerudi kwa Muumba akiwa ametimiza umri wa miaka 63, yaani miaka saba kabla ya ile inayosemwa kwenye vitabu vitakatifu kwamba maisha ya mwanadamu ni makumi mawili matatu (miaka 60) na kumi moja (jumla miaka 70) na kwamba baada ya hapo ni mateso tupu.

Mzee Mwenda ameacha majonzi makubwa na simanzi sio kwa familia yake tu, bali kwa wengi wetu tuliyemjua kwa karibu, kumfahamu na kufanya naye kazi katika tasnia ya habari kwa muda mrefu.

Kwangu alikuwa zaidi ya rafiki, maana alikuwa mshauri, mlezi, kiongozi, mhamasishaji, mburudishaji. Aliitenda kazi, akawavuta na kuwavutia wengi, kazi ngumu ameikamilisha.

Navuta picha namna nilivyomfahamu Mzee Peter Mwenda karibu miaka 24  unaelekea wa 25 sasa, kuanzia mwaka 1999 wakati nikiwa bado kijana mdogo nilipoingia katika Kampuni ya Business Times Limited (BTL), wachapishaji wa magazeti ya Majira, Spoti Starehe, Sanifu, Maisha na gazeti la Kiingereza la Business Times.

Tukio la haraka lililonijia mawazoni kuhusu kifo cha Mzee huyu ni ushauri wake kwa waandishi wa habari wenzake, baada ya yeye kujenga nyumba yake Kitunda-Kivule, Dar es Salaam na kuhamia mwaka 2000 na kisha kuwahamasisha waandishi zaidi ya 100 kununua viwanja Kitunda-Kivule ili wajenge nyumba kwa ajili ya kuishi.

Bila kumung’unya maneno nilikuwa kijana wa kwanza kufuata ushauri wake mwaka 2002 aliponishawishi ninunue eneo Kitunda-Kivule, alishawishi wengi lakini karibu 20 walikubali nikiwa miongoni mwake, alitamani sana kuwe na Mtaa ambao wangeishi waandishi wa habari.

Wapo baadhi walinunua na kujenga kutokana na kile walichokiita ‘kuepuka kero’ ya Mzee Mwenda, kwani  baada ya kuhamasishwa kununua tuliona ni porini wakatelekeza maeneo.

Lakini kwa vile marehemu Mwenda alijua maeneo ya kila mmoja wetu, akawa anapitia kuyakagua kila wakati na lazima akupigie simu kukueleza ukichelewa kujenga watu watayauza na asingekuwa muadilifu nina imani angeweza kuyauza, kwani baadhi yetu tulisahau hata yalipo maeneo hayo kutokana na kutoenda kutembelea mara kwa mara.

Waliotii maelekezo yake walijenga haraka, bahati nzuri wakati huo vipato tulikuwa tunafahamiana, wale ambao hawakumsikiliza baadhi waliuza maeneo yao, wale waliokataa kununua waliposhtuka na kuona umuhimu huo wakimuulizia tena tayari Kitunda-Kivule umeshakuwa mji mkubwa na gharama zake hazishikiki. Wote leo tunamkumbuka kila mmoja kwa namna yake.Sitausemea moyo wa mtu.

Baadhi ya waandishi wengine ambao walishawishiwa na Mwenda na wakanunua maeneo  Kitunda na walikuja nyuma yangu, ambapo mikataba yao ya mauziano wakati huo shahidi akiwa yeye ni Abdallah Mweri, Frank Sanga, Kulwa Mzee, Grace Michael, Jesse John, Spear Patrick, Reginald Miruko, Fred Majaliwa na  marehemu Shadrack Sagati kuwataja kwa uchache.

Ndoto yake ya kutaka waandishi wawe na eneo lao waishi hapo aliendelea kulishikilia wakati akiwa Ofisa Habari wa Shirikisho la Wasanii Tanzania (Shiwata), ambapo walianzisha Kijiji cha wanamichezo na wasanii huko Mwazenga, Mkuranga mkoani Pwani na wakiwa na eneo kubwa kwa ajili ya kuwapa viwanja wanamichezo, wasanii na waandishi wa habari.

Marehemu Mwenda alituhamasisha kwa kiasi kikubwa waandishi akasisitiza waende huko kwani maeneio yapo ya kutosha na tofauti na ilivyokuwa Kitunda-Kivule, kule Mkuranga gharama zilikuwa ndogo, jambo ambalo pia aliwaaambia wasanii na wanamichezo karibu wote aliowafahamu.

Wapo walioenda walipata maeneo ya kutosha, lakini kama ilivyo kawaida wapo ambao walienda wakapewa maeneo wakayatelekeza hawakurudi tena kwa maelezo kuwa ni mbali.

Bahati mbaya mhamasishaji amekwenda, lakini pia maeneo hayo tofauti na ilivyokuwa Kitunda ambapo alikuwa na afya njema, hivyo kuwa na nguvu yakuyatembelea mara kwa mara.

Kule Mkuranga bahati mbaya sikupata nafasi ya kwenda, lakini walioenda yalinunuliwa wakati tayari afya yake imeshaanza kutetereka, ninahofia baadhi yatapoea au yameshapotea. Hivyo wapo watakaolia kwa mengi, tuwape usaidizi wa kutosha.

    Jina la Buyoya

Mzee Mwenda alijulikana kwa majina mawili makubwa ya utani, waandishi wale wakongwe wa mwanzoni mwa miaka ya 1990 wakiongozwa na Mgosi Benny Kisaka walikuwa wakimuita Salehe Ghulum. Ghulum alikuwa Makamu Mwenyekiti wa klabu ya Simba, wakati wa uongozi wa Amir Ally Bamchawi, baadaye Ghulum alikuja kuwa Kaimu Mwenyekiti wa Simba baada ya kufariki Bamchawi.

Kizaazi cha waandishi wa habari za michezo cha mwishoni mwa miaka ya 1990 ambacho ndiyo akina siye na ndugu zangu Mahmoud Zubeiry, George John, Saleh Ally, Shija Richard, Ibrahim Bakari, Abdul Mohammed, Somoe Ng’itu, Honey Mohammed, Grace Hoka, Shinunu Amon, Bahati Mollel,Robert Komba kuwataja kwa uchache tulikuwa tunamuita Meja Pierre Buyoya.

Buyoya alikuwa Rais wa zamani wa Burundi aliyekuwa amejea madarakani Julai 1996, baada ya kumpindua Rais wa mpito Sylvestre Ntibantunganya. Alichukua madaraka kufuatia kifo cha Rais Cyprien Ntaryamirwa ambaye alikufa katika ajali ya ndege pamoja Rais wa Rwanda wakati huo Juvenal Habyarimana wakati wakitua uwanja wa ndege mjini Kigali, Rwanda 06 April 1994. Walikuwa wanatoka kwenye mazungumzo ya amani Arusha.

Hatua ya kumuita Buyoya ilitokana na ukaribu wake na baadhi ya wanachama wenzake wa Simba, ambao mwanzoni mwa mwaka 2000 waliiteka timu na kwenda kuificha Morogoro, miaka ile ambayo masuala ya mapinduzi katika klabu za Simba na Yanga ilikuwa jambo la kawaida

Pia Meja Buyoya ilitokana na mapinduzi yaliyofanywa na baadhi ya wanachama wa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo (TASWA) mwanzoni mwa Januari 2001 pale ukumbi wa Vatican Hotel na kutangaza kuuondoa uongozi halali wa Mwenyekiti Steven Rweikiza na Katibu Mkuu Mwina Kaduguda.

Hata hivyo mapinduzi hayo yalizimwa na Baraza la Michezo la Taifa (BMT), ambalo liliitisha Uchaguzi Mkuu uliofanyika Januari 27, 2021, ambapo Mobhare Matinyi alichaguliwa kuwa Mwenyekiti, Kaduguda Katibu Mkuu, Fred Ogot Makamu Mwenyekiti, Abdul Mohammed Katibu Mkuu Msaidizi na Juma Pinto akiwa Mhazini.

       Utani kwenye vyumba vya habari

Maisha yetu waandishi wa habari za michezo miaka ya 1990 yalikuwa ya furaha sana. Utani mwingi na kazi kazi. Mzee Mwenda alikuwa anapenda utani. Na utani ulianzia news room mpaka mtaani.

Tulitaniana kuanzia news room Majira lakini hata tulipotoka nje kukutana na waandishi wenzetu kutoka newsroom nyingine utani uliendelea na ulikuwa unatuunganisha hasa.

Yeye alipenda kuniita mimi Mgosi. Dawati letu la michezo lilikuwa na Mzee Jabir Idrisa, Masoud Sanani, Godfrey Lutego, Boniface Wambura, Frank Sanga, marehemu Willy Edward, Shija Richard, Dina Ismail na Ndaya Kassongo.

Karibu kila mtu alikuwa na jina lake la utani, wengine hawakuyapenda majina yao, lakini utani huo ulituunganisha sana katika kufanya kazi kwa upendo na amani na hali ilikuwa hivyo hata katika vyumba vingine vya habari.

Vitisho vya Prof. Maji Marefu

Nakumbuka wakati fulani mwanzoni mwa miaka ya 2000, promota maarufu wa ngumi, ambaye baadaye alikuja  kuwa Mbunge wa Korogwe Vijijini, Steven Ngonyani ‘Prof. Maji Marefu’, (alikuwa pia mganga wa kienyeji), alitupiga mkwara pale Manzese Friends Corner kwamba kuna mwandishi alijifanya kidume aliondoka na dada mmoja ambaye alikuwa msaidizi wake, hivyo alitoa muda wa saa tano tu aende akaombe radhi, vinginevyo ‘hatua kali’ zingechukuliwa  dhidi yake. Elewa neno hatua kali.

Hali ya huyo mwandishi ilikuwa mbaya sana, alikosa amani na muda ule uliotolewa na Prof. Maji Marefu mganga wa jadi tena kutoka Tanga, lakini kikubwa alikuwa anatulinda kiuchumi ulipita, hali iliyomfanya mwandishi yule awe amekosa amani.

Mikwara ya Prof. Maji Marefu ilikuwa mizito, alitishia kuhamisha sehemu za siri za mhusika kwa njia ya kishirikiana. Sitaki kukumbuka na kulimalizia hilo tukio. Nitalihadithia siku nyingine uhai ukiwepo. Huyo mwandishi yupo bado katika tasnia na ni mtu maarufu sana, ila itoshe kusema Mzee Mwenda na mwandishi Mashaka Mhando wa Tanga walitumia hekima kubwa sana kumtuliza Prof. Maji Marefu.

Shabiki wa Sikinde, rafiki wa Msondo

Mzee Mwenda alikuwa shabiki mkubwa wa bendi ya DDC Mlimani Park ‘Sikinde’, kila Jumapili alikuwa hakosi mwanzoni mwa miaka ile ya 2000 katika maonesho ya bendi hiyo ukumbi wa DDC Kariakoo.

Wimbo wake mkubwa aliopenda  ulikuwa Talaka Rejea, ilikuwa wakati Fulani tukienda pale DDC Kariakoo wakati huo wote tukiwa gazeti la Majira, alikuwa akiomba apigiwe wimbo huo.

Sikuwa nikifahamu nyimbo za zamani za dansi nyingi zilikuwa za vijembe, siku moja alinijulisha kuhusu wimbo huo wa Talaka Rejea kwamba kilikuwa kijembe kwa Msondo.

“Kwa nini mnadhani kilikuwa kijembe?’ Niliwahi kumuuliza wakati Fulani katika makala zangu za muziki miaka ya nyuma na nanukuu sehemu ya  majibu yake katika makala hiyo kwenye gazeti la Majira.“Ni kwa sababu Shaaban Dede alipoondoka Msondo alifuatwa Kariakoo mchana kweupe na kunyang’anywa shati ambalo Msondo walidai lilikuwa lao. Habari za aina hii husambaa haraka sana jijini Dar es Salaam, hasa kwenye vijiwe mchana, lakini jioni kwenye kumbi za dansi.

“Hii ilisambaa na baada ya muda ndipo Sikinde wakatoa kibao hicho, mtunzi akiwa ni Dede, mtu mwenye sauti kali aliyokuwa akiipandisha sana na kuimba kwa hisia kubwa, huku akishangiliwa na washabiki wake, ambao hata leo wapo baadhi Sikinde na wengine Msondo, maana hizi ndizo bendi kubwa na kongwe zilizobakia Tanzania.

“Katika wimbo huo Dede anasema: “Ulinitaliki kwa talaka rejea, bila aibu ulininyang’anya nguo mbele za watu …huku ukitoa kashfa nikajifunze kwa wazazi wangu …leo unaniambia nirejee kwako, ulivyonidhalili umesahau …mtu anapochukia, moyo kuurudisha furahani ni vigumu …ukweli nasema aheri nipate tabu kuliko kurejea kwako…”

“Tafsiri ikaja kwamba Dede alikuwa ameombwa na Msondo arejee kwao ndiyo maana akatoa maneno hayo, kwanza akizungumzia kunyang’anywa nguo mbele za watu, lakini pili akigusia suala la kutalikiwa, kudhalilishwa na kwamba kamwe hangerejea kwake.”

Nakumbuka Mzee huyu alinipeleka kwenye bendi za dansi ambako nilifanya makala na baadhi ya wanamuziki mahiri kwa nyakati tofauti, baadhi yao ni Muhidin Maalim Gurumo, Selemani Mbwembwe, Joseph Maina, TX Moshi William, Mustafa John Ngosha, Suleimani Mwanyiro, Tino Masenge,  Adam Bakari ‘Sauti ya Zege’ na Athuman Momba ambao wote wametangulia mbele ya haki.

Licha ya kuwa shabiki wa Sikinde, marehemu Mwenda alikuwa pia mdau wa Msondo Ngoma na rafiki wa karibu wa wanamuziki wa bendi hiyo, lakini wote walijua mapenzi yake yalikuwa Sikinde, ila alifanya kazi za Msondo vizuri tu.

         Ufahamu wa michezo

Hakika Mzee Mwenda alitumia vyema kalamu yake kuelezea mchezo na kumfanya yule aliyekuwa

hayupo kiwanjani kuelewa kilichotokea kwa ufasha, lugha mwanana na

vibwagizo viliomliwaza msomaji na kubaki kutabasamu kama vile alikuwa

kiwanjani anaangalia ule mchezo.

Kwenye mpira wa miguu naweza kusema sio tu alielewa alichokiona bali pia kufahamu mfumo ambao timu ilikuwa inatumia, uhodari na udhaifu wake, aliwafahamu wachezaji vizuri sana. Ila hakupenda kujikweza.

Wakati fulani mwandishi mkongwe Salim Said Salim alipata kuniambia kuwa miaka ya nyuma ilikuwa lazima mwandishi wa habari za michezo azielewe vyema timu ziliocheza na kuwajua wachezaji sio tu walipotokea bali wanaishi wapi na ni nani marafiki zao.

Pia alisema ilikuwa vizuri kujua na maeneo waliyopenda kutembelea, kwani hilo lilikuwa na umuhimu mkubwa zamani kwa vile mawasiliano hayakuwa rahisi kama hii leo ambapo simu za kiganjani zimesaidia sana kumpata mtu na kuzungumza naye.

Wakati mgumu kazini

Kama kuna wakati ambao nilikuwa na ugumu kazini, basi ni pale nilipoteuliwa kuwa Mhariri wa Habari za Michezo wa gazeti la Majira na miongoni mwa waandishi katika dawati langu ni Mzee Mwenda. Unatakiwa umtume mtu aliyekupokea, aliyekufundusha kazi, aliyekuonesha njia mbalimbali mjini. Lakini katika vyumba vya habari hayo ni mambo ya kawaida sana,

Nakumbuka siku moja jamaa mmoja ofisini alilalamika kwamba Mwenda habari zake za Simba tuziangalie sana kwani watu wanalalamika, nami nikamjibu kwa haraka kuwa hata yeye watu wanamlalamikia kuwa ni Yanga hivyo habari zake tuwe nazo makini sana. Ikawa sare ya bao 1-1.

Sijui kama alibadilika baadaye Mzee Mwenda, lakini wakati nafanya naye kazi katika chumba cha habari alikuwa rafiki wa kila mtu na kuheshimu mkubwa na mdogo.

Mwenda aliyeaacha mjane Elizabeth Mboma  aliyezaa naye watoto wanne, Joseph, John, Norbert na Kelvin, nilifanya naye kazi kwa karibu zaidi hadi nilipoondoka Majira Januari 2009 kujiunga na Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN), akiwa miongoni mwa watu wangu wa karibu niliowashirikisha kuhusu kuondoka kwangu.

  Kwaheri ya kuonana

Mzee Peter Mwenda aliyezaliwa Septemba 23,1960 katika Kijiji cha Masange, Kondoa mkoani Dodoma na kusoma Shule ya Msingi Chambalo na kisha sekondari Kinondoni Muslim Dar es Salaam, anazikwa leo mchana  nyumbani kwake Kitunda-Kivule, Dar es Salaam.

Jambo la  muhimu ni kuendeleza juhudi, ushupavu na umahiri aliouonesha marehemu katika maisha na kazini. Alikuwa muungwana aliyetimia, mchapa kazi, mstahamilivu na mtu mwenye upendo na aliyechukia fitna na husda.

Njia nzuri ya kumkumbuka ni kuishi maisha yake.

Yeye ametangulia na sisi tutafuatia.

Kwaheri Mzee Mwenda, kwaheri Meja Buyoya, kwaheri Ghulum. Nitakukumbuka daima. Umekuwa mwema kwangu na kwa wenzangu na sitakusahau maishani mwangu. Nilikuwa wako na ulikuwa wangu na zaidi ulikuwa mtu wa watu

Nenda Mzee Mwenda. Msalimie Kiona Mbali Conrad Dunstan, Willy Edward, Asha Muhaji, Innocent Munyuku, Cassian Malima, Willie Chiwango na waandishi wengine wengi ambao si rahisi kuwataja wote.

Umetuacha mkono, lakini daima tutakamatana mikono kukumbuka wema wako na ihsani uliyotendea wenzako na jamii ya waandishi wa habari, hasa wa fani ya michezo.

Sitakaa nisahau ushauri wako mzuri, huzuni yangu ni kubwa, lakini shukurani zangu ni kubwa zaidi. Daima ulikuwa na furaha, ulikuwa mtu mwema. Nenda kwa amani Peter Mwenda.

Kwaheri Peter… Peter… Peter kwaheri ya kuonana na Mwenyezi Mungu akulaze mahali pema peponi kaka yangu. Amina.🙏🏾🙏🏾🙏🏾

Habari Zifananazo

3 Comments
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button