ULIMWENGU mzima wa muziki unaomboleza kifo cha gwiji wa muziki, Tina Turner, ambaye alivuma kwa vizazi hadi vizazi. Tukio hili la kusikitisha linajiri miezi michache tu baada ya kufiwa na mwanawe mpendwa, Ronnie Turner.
Mwanamke huyu uthabiti na kipaji chake vilimfanya awe mfano wa kutazamwa na wengi. Umahiri wa sauti wa Tina Turner ulikuwa wa kutamanika na kila alipochukua maikrofoni na kuruka stejini aliwazingua mashabiki kwa njia ya kipekee.
Kwa sauti yake nyororo na yenye nguvu isiyo na kifani, alisisimua kwa nyimbo ambazo zilikuja kuwa za asili zisizoisha wakati. Kuanzia vibao kama “Simply the Best” hadi “What’s Love Got to Do with It”, Tina Turner alielewa kwa kina masuala ya muziki ambao daima utakumbukwa na vizazi hadi vizazi.
Alijizolea sifa nyingi katika kazi yake yote, ikiwa ni pamoja na Tuzo nyingi za Grammy, kutambuliwa kwa Heshima za Kituo cha Kennedy mnamo mwaka 2005, na kuingizwa kwenye Jumba la Umaarufu la Rock and Roll mnamo 1991.
Maonesho yake mahiri ya jukwaa na uoneshaji vilikuwa vya kiwango cha dhahabu cha burudani ya moja kwa moja, na ushawishi wake unaweza kuonekana katika wasanii wengi waliofuata nyayo zake.
Ushindani na uwepo wake kwenye jukwaa la kusisimua ulimfanya kuwa mmoja wa waimbaji mashuhuri wa kizazi chake.
Ilikuwa safari ndefu na mara nyingi yenye uchungu kutoka utoto wenye matatizo akikulia katika maeneo ya mashambani ya Nutbush, Jimbo la Tennessee hadi umaarufu wa kimataifa.
Tunapomuaga msanii huyu wa kishua, tunaangazia maisha na kazi yake. Jina lake halisi ni Anna Mae Bullock japo tunamfahamu zaidi kama Tina Turner. Pamoja na kufahamika kama mtunzi na mwimbaji wa muziki, pia alifanya vyema kama mwigizaji wa filamu na mwandishi wa vitabu.
Alizaliwa Novemba 26, 1939 na alikuwa na dada zake wawili. Kwa kuzaliwa ni raia wa Marekani lakini mwaka 2013 alibadili nyaraka zake na kuwa raia wa Uswisi.
Akiwa binti mdogo alikuwa akiimba katika kwaya ya kanisani kwenye Kanisa la Kibabtisti huko Nutbush wakati akiishi na bibi yake ambaye alikuwa ameshika sana dini, na katika moja ya makala ya maisha yake yanayofahamika kama “I”, Tina alinukuliwa akisema wazazi wake hawakumpenda na hawakumhitaji.
Katika maisha yake ya ujana na kabla ya kuwa Tina Turner alishawahi kufanya kazi za vibarua kama vile nesi msaidizi katika hospitali huko St Louis, Missouri, na mfanyakazi wa ndani.
Katika harakati za kimuziki, safari yake ilianza baada ya kuvutiwa na mwimbaji Ike Turner ambaye alikuwa akiimba na bendi ya ‘Kings of Rhythm’.
Ilikuwa katika klabu ya usiku, ambapo yeye na dada yake walikuwa wamekwenda jioni, alipomwona Ike Turner akiimba na bendi yake. Anna Mae alipewa kipaza sauti na uchezaji wake ulimvutia sana kiasi kwamba ulimfanya kuombwa kuimba na bendi.
Wakati huo, alikuwa kwenye uhusiano na mpiga saxophone wa bendi hiyo, Raymond Hill, ambaye alizaa naye mtoto, Raymond.
Alifanya rekodi yake ya kwanza kama mwimbaji msaidizi mnamo 1958, lakini nafasi yake kubwa ilikuja miaka miwili baadaye kwenye wimbo uitwao Fool in Love, ulioandikwa na Turner kwa ajili ya msanii Art Lassiter.
Wakati mwimbaji Art Lassiter aliposhindwa kujitokeza kwa ajili ya kurekodi, Anna Mae aliombwa kujaza nafasi kwa nia ya kwamba sauti zake zitaondolewa baadaye. Lakini DJ ambaye alisikia onesho hilo alifurahishwa sana, aliipitisha kwa lebo ya rekodi ya ndani.
Tangu siku hiyo maisha yake yalibadilika. Wimbo huo ulinunuliwa kwa dola 25,000 kama malipo ya awali tu jambo lililomfanya Ike Tuner kumbatiza jina la stejini “Tina”. Hatua hii ilibuniwa kuzuia wapenzi wa zamani kumfuatilia.
Fool in Love ilifika nambari 27 kwenye chati za Billboard na iliyofuata, ‘It’s Gonna Work Out Fine’, iligonga 20 bora na kuwashindia wawili hao Tuzo ya Grammy.
Baadaye Ike Turner alimwongezea jina lake la mwisho ‘Turner’ kisha akamsajili kisheria ili kulinda haki zake endapo mwanamuziki huyo angetaka kujiondoa chini ya menejimenti yake.
Endapo angeondoka basi jina la Tina Turner bado lingebaki kuwa hakimiliki ya Ike na angemuweka msanii mwingine yeyote kwa jina hilo hilo. Hivyo kuanzia hapo Anna Mae Bullock akatambulika rasmi katika jukwaa la muziki kimataifa kama Tina Turner.
Baadaye Tina aliolewa na Ike Turner ambaye alikuwa ametalikiana na mke wake wa tano. Wenzi hao hatimaye walifunga ndoa mnamo 1962 na baada ya takribani miongo miwili ya kufanya kazi na mume wake aliyemshutumu kwa unyanyasaji waliachana, ambapo Tina alibaki na magari mawili tu pamoja na jina lake.
Baada ya kuachana, Tina aliibuka kama msanii wa kujitegemea na akawa mmoja wa wasanii wakubwa wa pop wa miaka ya 1980 na albamu yake ya ‘Private Dancer’ iliyorekodiwa London, ilitoa vibao saba vya chati na kuzindua ziara kuu ya dunia.
Alirejea kwenye skrini miaka miwili baadaye kama Aunty Entity katika filamu ya Mad Max Beyond Thunderdome, na akachangia kwenye wimbo wa sauti wa filamu hiyo, ikijumuisha wimbo ‘We Don’t Need Another Hero’.
Mafanikio yaliendelea katika muongo uliofuata, ikiwa ni pamoja na kurekodiwa kwa GoldenEye, wimbo wa mandhari wa filamu ya kwanza ya James Bond ya nyota Pierce Brosnan.
Mwanzoni mwa karne, na akiwa na umri wa miaka 61, alitangaza kuwa anaenda kustaafu.
Tina Turner alisifiwa kama alama ya wanawake na mwaka 2003 alihudhuria tukio la Kennedy Center Honours ambapo nyota kama Oprah Winfrey, Al Green na Beyonce waliungana na Rais George Bush kutoa heshima.
Alirejea mwaka wa 2008, akiimba kwenye Tuzo za Grammy na kuanza ziara ya kusherehekea miaka yake 50 kama mwimbaji. Licha ya umri kuwa mkubwa nguvu zake zilionekana kutopungua na sauti ikiwa na nguvu kama zamani.
Mnamo 2013, akiwa na umri wa miaka 73, alikuwa mtu mzee zaidi kuwahi kuoneshwa kwenye jarida la Vogue.
Makala haya yametokana na vyanzo mbalimbali vya habari.
0755 666964 au bjhiluka@yahoo.com
mwisho
Comments are closed.