Burundi yalaumu matumizi mabaya ya ngoma

SERIKALI imelaani kile ilichodai ni ‘matumizi mabaya ya ngoma ya kitamaduni na takatifu’ katika tamasha lililofanyika wiki iliyopita nchini Uganda.

Katika ujumbe wa Twitter, Wizara ya EAC, Utamaduni na Michezo ilisema: “Burundi inafahamu matumizi mabaya ya Ngoma Takatifu ya Burundi wakati wa Tamasha  hilo…  Wizara inayosimamia Utamaduni inaarifu maoni ya kitaifa na kimataifa kwamba kamwe haitamvumilia yeyote anayekiuka tamaduni na desturi za Burundi.”

Haya yalikuja baada ya picha kuibuka kwenye mitandao ya kijamii zikiwaonesha wanawake wakicheza ngoma kwenye tamasha hilo.

Advertisement

Katika utamaduni wa Burundi, wanawake hawaruhusiwi kucheza ngoma na wanaruhusiwa kucheza tu wakiwa wamevalia mavazi maalumu.

Kwa mujibu wa Agizo la Rais la 2017 kuhusu ngoma ya Burundi, Kifungu cha 21 cha amri hiyo kinaonesha kwamba promota au kikundi kitakachoonesha ngoma bila kibali kinaweza kuadhibiwa kwa kusimamishwa kuonesha ngoma kwa miezi sita na kupigwa faini ya Faranga za Burundi (Fbu) 1,000,000 (takribani Dola 490).

“Kifungu cha 22: Bila kuathiri Kifungu cha 20, Wizara ya Utamaduni katika mamlaka yake inaweza kutekeleza vikwazo katika tukio la unyonyaji usiofaa wa kipengele hiki cha kitamaduni.”

Ngoma ya kitamaduni ya Burundi ya ‘Umurisho w’ingoma’ na ngoma ya kifalme imeandikwa katika orodha ya Unesco ya urithi wa utamaduni usioshikika (ICH).