Busti Kipaji yatabiriwa makubwa

OFISA Michezo kutoka Manispaa ya Ubungo, Mikansia Mwanga amesema kupitia kampeni ya ‘Busti Kipaji’ ameona baadhi ya vijana wenye vipaji na kwamba endapo wataendelezwa zaidi watafikia ndoto zao na kuwa wachezaji wa timu ya taifa Tanzania ‘Taifa Stars’.

Akizugumza wakati wa kuhitimisha kampeni hiyo leo Februari 20, 2024, Mikansia aliyemwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Hashim Komba amesema kampeni hiyo iliyoandaliwa na kampuni ya simu ya Tecno na kampuni ya mawasiliano ya simu Airtel iliyolenga kuibua vipaji vya vijana imekuwa na matokeo chanya.

“Kuna vijana wadogo lakini wanaonesha kwamba wana vipaji na vikiendeleza zaidi ya hapa, watakuwa ni vijana wazuri na tutapata vijana wa timu ya taifa” Amesema Mikansia.

Meneja Masoko wa Tecno Tanzania, Salma Abeid amesema kupitia tamasha hilo licha ya kupata washindi lakini wameunga mkono mahitaji ya viatu vya mpira kwa baadhi ya vijana waliokuwa na uhitaji.

“Ilikuwa ni kero kubwa ya watoto katika mazoezi na michezo yao, tumetoa pesa, medali, jezi tumetoa vitu mbalimbali ambavyo vitawasaidia baadaye katika michezo yao.”amesema Salma.

Balozi wa Busti Kipaji ambaye ni golikipa wa Simba na ‘Taifa Stars’ Aishi Manula amesema kampeni hiyo imekuwa fursa nzuri kwa vijana hao ambao pengine wengi wao walishindwa kutimiziwa mahitaji hayo na wazazi wao.

“ Sio vijana wote au watoto wote ambao wanaweza kupata viatu kutoka kwa wazazi wao, kulingana na watanzania asilimia kubwa tuna hali ya chini, wazazi wanatamani kusaidia vijana wao, watoto wao lakini kulingana na ugumu wa maisha wanashindwa kuwasaidia”. Amesema Manula.

Kampeni hiyo ni katika kuunga mkono jitihada za Serikali kuinua vipaji vya vijana, ikumbukwe pia Rais Samia aliwahi kuzungumza suala hilo ambapo aliandaa mashindano ya ‘Samia Cup’ yaliyofanyika mwaka 2023 Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro ambayo yalilenga kuibua vipaji vya vijana.

Habari Zifananazo

Back to top button